KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, jioni ya leo imeendeleza wimbi la ushindi kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), safari hii ikiichapa Toto African bao 1-0.

Ushindi huo umeifanya Azam FC kuandika rekodi mpya ya kushinda kwa mara ya kwanza ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza dhidi ya Toto African tokea mabingwa hao waanze kucheza Ligi Kuu msimu wa 2008/2009.

Huo ni mchezo wa 13 timu hizo kukutana, Azam FC ikiongeza rekodi ya ushindi ya mechi saba, Toto ikishinda mara mbili na iklishuhudiwa wakienda sare mara nne.

Mbali na rekodi hiyo, ushindi huo pia umeifanya Azam FC kupanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikifikisha jumla ya pointi 22 sawa na Stand United iliyoishusha kutokana na kuwa na tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Azam FC ilibidi isubiri hadi dakika ya 81 kufunga bao hilo pekee, lililowekwa kimiani na mshambuliaji kinda, Shaaban Idd, aliyefunga bao hilo kwenye mazingira magumu baada ya kukabwa na mabeki wawili wa Toto, akitumia vema pasi safi ya nahodha John Bocco, aliyewazidi maarifa mabeki wa timu hiyo.

Hilo ni bao la kwanza la kinda huyo aliyelelewa kwenye kituo cha kukuza vipaji cha Azam FC ‘Azam FC Academy’, tokea apandishwe timu kubwa mwishoni mwa msimu uliopita, ambapo hii ni mechi ya pili mfululizo anaibuka shujaa kufuatia mchezo uliopita kutoa krosi safi iliyozaa bao la ushindi dhidi ya Kagera Sugar (3-2).

Kipindi cha kwanza mchezo haukuwa na kasi sana tofauti na kipindi cha pili, ambapo Azam FC ilifanikiwa kupeleka mashambulizi kadhaa langoni mwa Toto African kufuatia mabadiliko yaliyofanywa ya kuingia Idd na kutoka Khamis Mcha.

Mbali na Azam FC kufunga bao ilifanikiwa kutengeza nafasi kadhaa ambazo zilishindwa kutumiwa vema, ya kwanza ikiwa ni ile aliyoikosa Khamis Mcha, dakika ya 19 baada ya kuukosa mpira kufuatia krosi iliyopigwa na Mudathir Yahya.

Mcha alikaribia kuipa bao la uongozi Azam FC dakika ya 31, baada ya kupiga faulo nzuri iliyokuwa ikielekea nyavuni lakini kipa wa Toto African, Mussa Kirungi, alifanya kazi ya ziada kwa kuupangua mpira huo kabla haujaokolewa na mabeki.

Kikosi cha Azam FC leo:

Aishi Manula, Erasto  Nyoni, Gadiel Michael, Daniel Amoah, David Mwantika, Frank Domayo, Khamis Mcha/Shaaban Idd dk 46, Salum Abubakar, John Bocco (C), Mudathir Yahya/Francisco Zekumbawira dk 67, Ramadhan Singano/Gonazo Ya Thomas dk 57