KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Zeben Hernandez, ameweka wazi kuwa wana kazi moja tu kwenye mchezo wa kesho Jumatano dhidi ya Toto African kuhakikisha wanapambana na kuondoka na pointi tatu muhimu.

Mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utafanyika ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na tayari kikosi cha Azam FC kimewasili mjini hapa tokea Jumamosi iliyopita jioni.

Mbali na kucheza na Toto, pia kikosi hicho kitacheza na Mbao FC Jumapili ijayo ndani ya dimba hilo kabla ya kumalizia mechi zake za mzunguko wa kwanza wa ligi kwa kukipiga na Mwadui ya Shinyanga Novemba 9 mwaka huu ndani ya Uwanja wa Mwadui.

Hernandez ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya mwisho ya kujiandaa na mchezo huo leo asubuhi, kuwa anatarajia upinzani mkali kutoka kwa wapinzani wao licha ya timu hiyo kuwepo nafasi mbaya kwenye msimamo wa ligi.

“Mchezo wa kesho ni mchezo ambao utakuwa na umuhimu wa kipekee, kwa sababu ni miongoni mwa michezo ambayo imetufanya tuje Kanda ya Ziwa kucheza, na lengo ambalo limetufanya kuja huku ni kukusanya pointi nyingi kadiri inavyowezekana,” alisema.

Huo utakuwa ni mchezo pili wa timu hiyo msimu huu kucheza kwenye Kanda ya Ziwa, ambapo wa kwanza ulikuwa ni ule wa Ijumaa iliyopita walioichapa Kagera Sugar mabao 3-2 ndani ya Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Kagera.

Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania, alisema kuwa hawezi kuwadharau wapinzani wake kutokana na nafasi ya 15 wanayoshika kwenye msimamo wa ligi.

“Kiufupi timu tunayocheza nayo tunapaswa kuiheshimu, ukiangalia kwamba wako kwenye nafasi mbaya kwenye msimamo wa ligi, lakini ukingalia pia rekodi zao wanaweza kuja kutumia nafasi hiyo kucheza kwa bidii ili kuweza kupata ushindi kwa upande wao, lakini kikubwa zaidi tunajaribu kupambana kadiri inavyowezekana ili kupata ushindi,” alisema.

Azam FC itaingia dimbani ikiendelea kuwakosa nyota wake watatu, mabeki Bruce Kangwa, Shomari Kapombe ambao ni majaeruhi huku Nahodha Msaidizi Himid Mao akiendelea kutumikia adhabu yake ya kadi nyekundu.

Takwimu zao msimu huu

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi kinacholainisha koo na kuchangamsha mwili cha Azam Cola pamoja na Benki Bora Nchini kwa usalama wa fedha zako ya NMB, imeshacheza jumla ya mechi 12 za ligi ikishinda tano, sare nne na kupoteza tatu na imejikusanyia pointi 19 ikizidiwa pointi 13 na kinara wa ligi Simba aliyekuwa nazo 32.

Toto African kwa upande wao wanashika nafasi ya 15 kwenye ligi baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 11 katika michezo 13 waliyocheza, ikiwa imeshinda mara tatu, sare mbili na kupoteza nane.

Rekodi zao (H2H)

Kihistoria timu hizo zimekutana mara 12 kwenye mechi za ligi tokea msimu wa 2008/2009, Azam FC ilipocheza kwa mara ya kwanza Ligi Kuu baada ya kupanda daraja.

Azam FC ndio inarekodi bora zaidi kwa mechi hizo zote walizocheza, ikiwa imeshinda mechi sita kati ya hizo zote ndani ya uwanja wa nyumbani huku Toto ikishinda mara mbili kwenye Uwanja wake wa nyumbani CCM Kirumba na mechi nne zikienda sare.

Mechi hizo zote walizoenda sare zilifanyika Uwanja wa CCM Kirumba, hivyo takwimu zinaonyesha kuwa Azam FC haijawahi kupata ushindi ndani ya uwanja huo, ambapo katika mechi sita walizocheza hapo imeweza kutoa sare nne na kufungwa mara mbili na wenyeji wao hao.

Jumla ya mabao 33 yamefungwa kwenye mechi hizo 12, wastani wa kufunga mabao ukiwa ni mabao 2.75 katika mchezo mmoja, Azam FC ndio kinara ikiwa imetupia robo tatu ya mabao hayo ambayo ni 23 na Toto yenyewe ikifunga 10 tu.

Cha kufurahisha zaidi kwa upande wa Azam FC, ni mabingwa hao kuruhusu kufungwa mabao mawili tu katika mechi zake za nyumbani sita walizocheza na Toto African, ambayo imeshuka daraja mara moja tokea Azam FC ipande daraja.

Mechi zao zote walizocheza VPL. 

03/04/2016 Toto African 1-1  Azam FC 

01/11/2015 Azam FC       5-0  Toto African 

30/01/2013 Azam FC       3-1  Toto African

19/09/2012 Toto African  2-2  Azam FC

30/04/2012 Azam FC       3-1  Toto African

02/11/2011 Toto African  1-1  Azam FC

04/02/2011 Azam FC       3-0  Toto African

18/09/2010 Toto African  1-0  Azam FC

26/01/2010 Azam FC       1-0  Toto African

27/08/2009 Toto African  2-2  Azam FC

26/04/2009 Toto African  1-0  Azam FC

24/09/2008 Azam FC       2-0  Toto African