KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imekuwa gumzo kubwa jijini Mwanza kwenye mitaa inayokatisha kuelekea mechi mbili zijazo itakazocheza jijini humo dhidi ya Toto African keshokutwa Jumatano na Mbao FC Jumapili ijayo.

Mashabiki wengi wamekuwa wakinukuliwa mara kwa mara kila basi la Azam FC linapokatisha, wakipiga miluzi kuashiria shangwe na asilimia kubwa wakiwataja jina la nahodha wa timu hiyo, John Bocco na staa wa zamani wa kikosi hicho, Kipre Tchetche.

Jambo la kuvutia zaidi lililotokea kwenye mazoezi ya leo Jumanne jioni yaliyofanyika Uwanja wa Chuo cha Ualimu cha Butimba, ni wanachuo na baadhi ya wakazi wa eneo hilo la Butimba mkoani hapa, kuvamia uwanjani mazoezi yalipoisha na kuwakimbilia nyota wa Azam FC na kuanza kupiga nao picha wengine wakipiga ‘selfie’ za kutosha na kurekodi video.

Wachezaji wa Azam FC walionekana kufurahishwa na mashabiki hao na hapo ndipo zilipoanza shangwe kwa mashabiki hao kushikwa na furaha isiyo na kifani kwa muda wa dakika 15 za tukio hilo, wakidai kuwa wanashukuru sana kuonana ana kwa ana na wachezaji hao ambao walikuwa wakiwaona kwenye televisheni tu.

Moja ya vitu vilivyowavutia sana ukiondoa wachezaji wa kikosi hicho, ni basi la kisasa linalotumiwa na kikosi hicho aina ya Higer, wakidai kuwa Azam FC ni timu bora nchini inayoendeshwa kisasa huku wengine wakilizunguka na kupiga nalo picha za ukumbusho.

Ukiondoa tukio hilo la mashabiki, kiujumla mazoezi ya Azam FC yalikuwa mazuri leo licha ya kuwepo changamoto ya uwanja, ambapo wachezaji walionekana kuyafurahia na kufanya programu ya leo kwa bidii kubwa.

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi kinacholainisha koo cha Azam Cola na Benki bora kabisa kwa usalama wa fedha zako ya NMB, itafanya mazoezi yake ya mwisho kesho jioni ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba kabla ya kuvaana na Toto African Jumatano ijayo.