VIJANA 12 kutoka mkoa wa Morogoro na Dodoma wamechaguliwa kwenye mchujo wa kusaka vijana wenye vipaji chini ya umri wa miaka 17 (U-17) ulioratibiwa na Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC ndani ya Uwanja wa Jamhuri, Morogoro jana.

Zoezi hilo linalosimamiwa na Mkuu wa Maendeleo ya Soka la Vijana Azam FC, Tom Legg raia wa Uingereza, lilihusisha vijana 528 huku 32 kati ya hao wakiingia fainali kabla ya kuchujwa na kupatikana waliobora zaidi 12.

Vijana hao 12 wanafanya idadi kamili ya vipaji vilivyochaguliwa kwenye mchujo wa awali kufikia 37 kati ya vipaji 2,073 vilivyofanyiwa usaili, wengine wakipatikana mikoa miwili ya awali ya Dar es Salaam na Tanga.

Sasa ni zamu ya Zanzibar

Wikiendi hii zoezi hilo la kusaka vipaji litaendelea tena kwa kufanyika Kisiwani Unguja, Zanzibar ndani ya Uwanja wa Amaan, Jumamosi ijayo Novemba 5 kuanzia saa 1.00 asubuhi hadi saa 9.00 Alasiri.

Kama umezaliwa mwaka 2000, 2001 au 2002 na unaishi Zanzibar katika Visiwa vya Unguja na Pemba, unaombwa kufika kwenye majaribio hayo ya sita kufanyika.

Tafadhali unaombwa kufika na nakala ya cheti chako cha kuzaliwa kwa wale wote watakaokuja kwenye majaribio hayo.

Kwa majaribio mengine ya wazi kuhusu sehemu, tarehe na muda, tutawatangazia hivi karibuni.

Tafadhali washirikishe rafiki zako ujumbe huu!