BEKI kinda wa kushoto wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Gadiel Michael, amesema kuwa mechi mbili mfululizo alizoanza kikosi cha kwanza zimempa ari mpya ya kuendelea kujituma na kupambana zaidi ili aweze kupewa nafasi ya kuendelea kucheza.

Michael mpaka sasa amefanikiwa kucheza kwa jumla ya dakika 169 kwenye mechi hizo dhidi ya JKT Ruvu aliyocheza kwa dakika zote 90 huku ile ya juzi na Kagera Sugar akitolewa dakika 79 na kuingizwa winga Khamis Mcha ili kuongeza zaidi mashambulizi. 

Kwa ujumla ameweza kukonga nyoyo za mashabiki wa timu hiyo pamoja na benchi la ufundi kwa muda mchache huo aliocheza kutokana na kasi yake ya kupanda kusaidia mashambulizi na kurudi kwenye eneo lake la ukabaji.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Michael alisema kuwa kwa kiasi kikubwa amefanikiwa kutimiza kile benchi la ufundi ilichokuwa inakihitaji na ndio maana ameendelea kupewa nafasi zaidi ya kuwemo kikosini.

“Hii ni nafasi ya pili nimeweza kupata, hii inanipa morali mimi kama mimi kuweza kuendeleza juhudi na kuendeleza kile kitu ambacho nazidi kukionyesha ili mwalimu aweze kuendelea kuniamini.

“Namshukuru Mungu ni bahati ambayo nilikuwa naihitaji muda mrefu sana ili niweze kupata nafasi, nashukuru Mungu nimeweza kuitumia vema kwa kuonyesha mechi ya kwanza na ile ya pili naamini atazidi kunijalia zaidi kuendelea kufanya vizuri,” alisema.

Kinda huyo aliyelelewa kwenye kituo cha kukuza vipaji cha Azam FC ‘Azam Academy, aliwaambia mashabiki wa timu hiyo kuwa waendelee kumuamini kwani ataendelea kupigana ili waendelee kufanya vizuri katika mechi zijazo huku akiwaahidi mambo makubwa zaidi.

“Mashabiki wa Azam FC mimi naomba wategemee kitu kikubwa zaidi kutoka kwangu, nimekuja kwa ari mpya kwa sababu mtu yoyote anayegombea nafasi akija kuipata basi anajitahidi kadiri awezavyo aweze kuisaidia timu yake kupata ushindi, naomba waendelee kuniamini na kunikubali kuwa mimi ninaweza,” alisema.

Amfurahisha Zeben

Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, hakuwa nyuma kusifia kiwango kizuri cha nyota wake huyo kinda, akidai kuwa atazidi kumsaidia kwa kumchezesha ili kukuza zaidi kiwango chake.

“Mchezo wa kwanza aliocheza ulifanikiwa kunipa imani zaidi juu yake, hata mechi ya pili pia, Gadiel ni mchezaji mdogo ambaye anapaswa kusaidiwa lakini kiwango chake ni kikubwa, tutaendelea kumsaidia kwa kumchezesha kwa sababu analeta mabadiliko makubwa kwenye timu,” alimaliza Hernandez wakati akiongea kwa msisitizo.

Ingizo la Michael kikosini linatokana na kuwa majeruhi kwa mabeki wawili wa pembeni wakongwe, Shomari Kapombe anayecheza upande wa kulia na Bruce Kangwa, anayecheza namba zote za upande wa kushoto pamoja na nafasi ya ushambuliaji.

Kikosi cha Azam FC tayari kipo kambini jijini Mwanza katika Hoteli ya Royal Residence tokea jana jioni baada ya kuwasili kutokea Kagera, kikijiandaa na mechi mbili mkoani humo, ya kwanza ikicheza Jumatano ijayo Novemba 2 dhidi ya Toto African kabla ya kuivaa Mbao FC Jumapili ijayo Novemba 6, mechi zote zikipigwa Uwanja wa CCM Kirumba.

Kuelekea mechi ya Toto, kikosi hicho kinatarajia kuanza mazoezi jioni ya leo ndani ya uwanja huo, kitaendelea tena kesho jioni na Jumanne muda huo huo kabla ya kumvaa mpinzani wake huyo.