KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, tayari kimewasili salama Jijini Mwanza jioni hii kikitokea mkoani Kagera, kikiwa na morali kubwa kuondoka na pointi zote sita.

Azam FC ikiwa jijini hapa itacheza mechi mbili za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Toto African Jumatano Ijayo (Novemba 2) na Mbao FC Jumapili Ijayo Novemba 6, zote zikifanyika Uwanja wa CCM Kirumba.

Mabingwa hao wanatua wakiwa wametoka kushinda ugenini jana baada ya kuichapa Kagera Sugar mabao 3-2, mabao ya Azam FC yakitupiwa nyavuni na Mudathir Yahya, Frank Domayo na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, aliyefunga la ushindi.

Wakiwa jijini hapa, Azam FC imefikia katika Hoteli ya Royal, ambapo kwa mujibu wa programu ya Kocha Mkuu Zeben Hernandez, kikosi hicho kinatarajia kufanya mazoezi mara tatu kabla ya kuivaa Toto, kikianza kesho na siku mbili zilizobakia Jumatatu na Jumanne ikifanya jioni muda utakaofanyika mchezo huo.