KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kutupa karata yake ya kwanza muhimu kesho Ijumaa kwenye mechi za mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kukipiga na wenyeji wao Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, mkoani Kagera.

Kuelekea mchezo huo muhimu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Kocha Mkuu wa mabingwa hao Zeben Hernandez, ameuambia mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa watakuwa na kazi moja tu ya kusaka pointi tatu katika kipute hicho.

“Ni mechi nzuri tunayotakiwa kuzoa pointi tatu, hali ya timu haipo vizuri sana kutokana na matokeo, lakini nafikiria kuwa mechi ya mwisho tuliyocheza na kupata ushindi ilibadilisha mawazo ya wachezaji, hivi sasa wanafikiria mambo mazuri.

“Malengo yetu ni kuendelea kuboresha kiwango cha timu na kushinda pointi tatu kesho, kwa sababu nafikiria kuwa mashabiki, wachezaji na Azam FC kwa ujumla wanahitaji pointi tatu,” alisema Hernandez.

Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania, aliweka wazi kuwa katika mchezo huo atawakosa nyota wake watatu ambao ni mabeki Shomari Kapombe, Bruce Kangwa na kiungo Himid Mao, aliyepata kadi nyekundu kwenye mchezo uliopita dhidi ya JKT Ruvu.

Kapombe ambaye alitarajiwa kurejea dimbani kwenye mchezo huo, anapumzishwa baada ya kujitonesha nyama za paja kwenye mazoezi ya mwisho leo jioni, yaliyofanyika Uwanja wa Kaitaba, huku Kangwa akiwa na maumivu ya mbavu tokea timu ilipowasili mkoani hapa juzi.

Kwa upande wake nahodha wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, ameuzungumzia mchezo huo akisema kuwa wanamorali kubwa kuelekea mtanange huo kutokana na ushindi walioupata Jumamosi iliyopita.

“Kagera ni timu nzuri imeanza ligi vizuri lakini mchezo wao wa mwisho wametoka kupoteza naamini watatupa changamoto nzuri na sisi ukiangalia tumetoka kushinda mchezo uliopita kwa hiyo naamini morali yetu itakuwa ya ushindi zaidi kuliko hata hao Kagera,” alisema.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo, ikiwa inakamata nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 16, hivyo ushindi wowote kesho utaifanya kufikisha jumla ya pointi 19 na kupanda kwa nafasi mbili hadi ya nne ikizishusha Mtibwa Sugar (17) na wapinzani wao hao Kagera (18).