KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuendelea na mpango wake wa Kitaifa wa kusaka vipaji kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 (U-17) Jumapili hii Oktoba 30 mjini Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri kuanzia saa 1.00 asubuhi hadi saa 8.30 mchana. 

Majaribio ya mjini humo yatahusisha pia vijana kutoka mkoa wa jirani wa Dodoma, ambao wanaombwa kufika kwenye uwanja huo ili nao waonyeshe vipaji vyao.

Wikiendi inayofuata Jumamosi Novemba 5, tutafanya majaribio mengine ya wazi kwenye Uwanja wa Amaan, Unguja, Zanzibar  kuanzia saa 1.00 asubuhi hadi saa 9.00 Alasiri.

Kama umezaliwa mwaka 2000, 2001 au 2002 na unaishi Morogoro, Dodoma au Zanzibar, unaombwa kufika kwenye majaribio hayo ya wazi ya tano na sita.

Tafadhali unaombwa kufika na nakala ya cheti chako cha kuzaliwa kwa wale wote watakaokuja kwenye majaribio hayo.

Tayari zoezi hili limefanyika kwa mafanikio makubwa kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Tanga, ambako jumla tuliwafanyia majaribio jumla ya vijana 1,545 na kuvuna 25, ambao wataingia kwenye mchujo wa mwisho utakaofanyika baadaye mwaka huu ndani ya viunga vya Azam Complex, Chamazi.

Kwa majaribio mengine ya wazi kuhusu sehemu, tarehe na muda, tutawatangazia hivi karibuni.

Tafadhali washirikishe rafiki zako ujumbe huu!