KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo mchana imewafariji wakazi wa mkoa wa Kagera walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10 mwaka huu mkoani humo.

Tetemeko hilo mbali na kuharibu makazi ya watu taktribani 16,667, pia imeshuhudiwa wakazi 17 wa mkoa huo wakipoteza maisha kutokana na janga hilo la asili.

Katika kuwafariji waathirika, uongozi wa Azam FC ulioongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba na Makamu Mwenyekiti, Nassor Idrissa pamoja na wachezaji wa kikosi hicho, ulikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali Mstaafu, Salum Mustafa Kijuu, katoni 50 za maji ya Uhai pamoja na kumi za juisi.

Akiongea kwa niaba ya uongozi wa Azam FC mbele ya Mkuu wa Mkoa huyo, Kawemba alianza kutoa pole kwa waathirika wa tetemeko hilo, huku akieleza kuwa timu hiyo ni moja ya walioguswa na tukio hilo kutokana na mashabiki wao nao kuathirika.

“Tumeguswa kwa sababu sisi tunacheza mpira lakini washabiki wetu ni hao ambao walioathirika, humu ndani kuna watoto, kuna kinamama, kuna watu wazima, pia mashule yameathirika, majengo ya ibada.

“Hivyo pamoja na kwamba Kampuni kubwa ya Azam imeshakuja hapa kutoa msaada na kilichopatikana, lakini timu tumesema kwamba tukifika hapa tuwe sehemu ya watu ambao tumeguswa na suala hili, kwa hiyo tuna vitu vichache ambavyo tungependa kukabidhi pamoja na kuwaona waathirika kwani tumekuwa tukiyapata kwenye televisheni,” alisema.

Katika hatua nyingine, alichukua fursa hiyo kumkaribisha Mkuu wa Mkoa huyo kuhudhuria uwanjani mechi yao ya kesho Ijumaa dhidi ya Kagera Sugar, akidai kuwa watafarijika wakiona uwepo wake.

“Azam FC hatuna makundi yoyote anayetupenda sisi tunakwenda naye na hatubagui mashabiki wakuungana na sisi, lakini kwa yoyote mwenye nia njema anayetaka mpira wa Tanzania kusogea mbele sisi tunakwenda naye,” alisema.

Naye Kijuu alizipokea salamu zote za pole kwa wakazi wa mkoa huo, huku akiipongeza Azam FC kwa kuwa timu ya kwanza kusaiadia waathirika wa tetemeko hilo.

“Mimi ni mwanamichezo hivyo nikiona timu ya michezo kama hii ikija inanipa faraja kubwa mimi napenda sana, ni kweli mkoa wetu umepigwa na tetemeko, hivyo tuna pigo kubwa, tumeendelea kupata misaada mbalimbali hivyo nawakaribisha sana na nawashukuru,” alimalizia Kijuu.

Uongozi wa Azam FC pia ulipata fursa ya kutembelea baadhi ya maeneo yaliyoathirika pamoja na kukabidhi misaada hiyo, ambapo katika maongezi yake na waathirika ilishuhudiwa Kawemba akibubujikwa na machozi kutokana na kuguswa na tukio hilo pamoja na hali mbaya iliyopo kwenye baadhi ya makazi.

Waathirika hao waliipongeza sana Azam FC kutokana na jitihada zao walizofanya kupeleka misaada hiyo huku wakikiitakia kila heri katika majukumu yao ya kila siku.