BAADA ya kukosa mechi sita zilizopita za Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, beki wa kulia Shomari Kapombe anatarajia kurejea dimbani Ijumaa ijayo kuivaa Kagera Sugar.

Kapombe alikosekana kwenye mechi hizo kutokana na majeraha ya nyama za paja yaliyokuwa yakimsumbua, aliyopata kwenye mchezo dhidi ya Simba uliomalizika kwa mabingwa hao kupoteza kwa kufungwa bao 1-0.

Joto la utabibu la Azam FC chini ya mtaalamu wa viungo Sergio Perez Soto na Daktari wa timu, Mwanandi Mwankemwa, leo Jumatano asubuhi limemruhusu Kapombe kuanza mazoezi na wachezaji wenzake baada ya wiki iliyopita kumaliza programu ya mazoezi mepesi.

Soto ameuambia mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa Kapombe yuko vizuri hivi sasa na malengo yao makubwa ni kuwemo kwenye orodha ya wachezaji wa Azam FC watakoivaa Kagera Sugar katika mchezo wa raundi ya 13 ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

“Wachezaji wote wako vizuri kwenye kambi yetu hapa Bukoba (mkoani Kagera), isipokuwa wasiwasi upo kwa beki Bruce Kangwa ambaye anasikia maumivu ya mbavu,” alisema mtaalamu huyo.

Soto alisema wanatarajia kumfanyia vipimo vya X-Ray nyota huyo ili kujua undani wa tatizo lake na hapo ndipo watakapotoa ripoti juu ya majeraha yake.

Kikosi cha Azam FC kipo vizuri hivi sasa na makocha wote chini ya Kocha Mkuu Zeben Hernandez, wamekuwa wakifanya kazi kubwa kila siku kuzidi kukiboresha kikosi hicho na mwanga mkubwa umezidi kuonekana kadiri siku zinavyokwenda.

Mara baada ya kufanya mazoezi asubuhi, kikosi hicho kitaendelea na programu kali ya kujiweka vizuri kuelekea mchezo wa Kagera Sugar kwa kupiga mazoezi mengine jioni ya leo na kesho kitajifua mara ya mwisho kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba itakapofanyika mechi hiyo.

Malengo makubwa ya Azam FC ni kuendelea kufanya vizuri katika mechi zijazo kwa kuchukua pointi tatu kadiri iwezekanavyo ili kuzidi kuwafurahisha mashabiki wake na kujiweka vema kwenye msimamo wa ligi.