KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeendelea kuvuna mashabiki kila kukicha na safari hii habari njema ni kuwa leo imefanikiwa kujipatia takribani mashabiki 50 katika Chuo cha St Augustine, Tawi la Bukoba, mkoani Kagera.

Kikosi cha Azam FC hivi sasa kipo mkoani humo kikijiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) itakaocheza dhidi ya wenyeji wao Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaitaba keshokutwa Ijumaa.

Katika mazoezi ya kwanza leo asubuhi, waliyofanyia ndani ya uwanja wa chuo hicho, mamia ya mashabiki waliweza kushuhudia mazoezi hayo wakiwemo baadhi ya wanachuo hao waliojitambulisha kama mashabiki damu wa Azam FC.

Mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz ulipata fursa ya kuzungumza na mmoja wa wanachuo hao, Emmanuel Kaiza, ambaye amesema kuwa moja ya sababu kubwa iliyomfanya kuipenda na kuisapoti ni kutokana na timu hiyo kuendeshwa kwa uweledi wa hali ya juu.

“Azam FC ni timu ambayo inajielewa tofauti na timu nyingine ina uongozi mzuri, wachezaji wazuri na ina kila kitu kizuri na utaratibu wao wa kuiendesha timu unaeleweka, hakuna longolongo tulizoizoea kwa timu nyingine, kusema kweli ni timu ya Kimataifa,” alisema Kaiza huku akiungwa mkono na wanachuo wenzake.

Kaiza hakusita kuitabiria mema timu yake hiyo pendwa, akisema itatisha hapa nchini na kimataifa kwa miaka michache ijayo huku akidai ipo siku itakuja kuifikia na kuwa juu ya moja ya miamba ya Afrika, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DR Congo).

“Azam FC ni timu ambayo itakuja kufanya vizuri zaidi hapa ndani na Kimataifa kuliko timu nyingine, kwanza ukiangalia ina miaka michache tokea ianzishwe, mpaka sasa wana kiwanja chao, basi zuri la kimataifa, ila kuna timu nyingine hapa nchini zimeanza hata kabla ya Uhuru wetu lakini hawajawafikia Azam FC.

“Kwa kweli timu yangu inanipa imani kubwa ya kufikia kule walipo TP Mazembe na pia inaweza kuwa juu yao kabisa cha msingi nawaomba mashabiki wenzangu waendelee kuipa sapoti Azam FC na wengine wajitokeze zaidi kuishangilia na kuwa mashabiki wa timu hii ambayo inaendelea kuleta mapinduzi katika soka letu,” alimalizia shabiki huyo.

Mashabiki hao wameweka wazi kuwa kuelekea mchezo wa Kagera Sugar watajitokeza uwanjani kwa wingi kuishangilia Azam FC ili iweze kupata ushindi.

Mara baada ya kikosi hicho kumaliza mazoezi, mashabiki hao walipata fursa ya kupiga picha ya ukumbusho wakiongozwa na Mkuu wa Chuo hicho, Father Frowin Mlengule.

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi kinacholainisha koo cha Azam Cola na Benki bora nchini kwa usalama wa fedha zako ya NMB, imeendelea kupata mashabiki wapya kila kukicha kutokana na misingi mizuri waliyojiwekea ya kuongoza timu hiyo kisasa na kiuweledi.