JUMLA ya wachezaji 23 wa kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, wamesafiri na kikosi hicho kwa ajili ya mechi nne za mwisho za kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) zitakazochezwa kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Kikosi hicho kilianza safari jana alfajiri na kufikia mjini Kahama, Shinyanga kabla ya leo Jumanne asubuhi kuanza safari ya kuelekea Bukoba, mkoani Kagera kitakapocheza na wenyeji wao Kagera Sugar ndani ya Uwanja wa Kaitaba Ijumaa ijayo.

Nyota waliosafiri ni makipa Aishi Manula, Mwadini Ally, Metacha Mnata, mabeki Aggrey Morris, Daniel Amoah, Erasto Nyoni, David Mwantika, Gadiel Michael, Ismail Gambo na Shomari Kapombe, atakayejiunga na kikosi hicho leo akitokea Dar es Salaam.

Viungo ni Himid Mao, Salum Abubakar, Frank Domayo, Jean Mugiraneza, Mudathir Yahya, Ramadhan Singano, Bruce Kangwa, Khamis Mcha, Masoud Abdallah pamoja na washambuliaji John Bocco (C), Francisco Zekumbawira, Gonazo Bi Ya Thomas Renardo na Shaaban Idd.

Baada ya kumaliza mchezo huo, kikosi hicho kitaanza safari nyingine ya kuelekea mkoani Mwanza, kucheza mechi mbili dhidi ya Toto African (Novemba 2) na Mbao FC (Novemba 6), zote zikipigwa ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba.

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola kinachoburudisha koo na kusisimua mwili pamoja na Benki ya bora kabisa nchini kwa usalama wa fedha zako ya NMB, itamalizia mechi ya mwisho ya mzunguko wa kwanza wa ligi kwa kukipiga na Mwadui ya Shinyanga ikiwa ni mechi ya kiporo itakayofanyika Uwanja wa Mwadui Novemba 9 mwaka huu.

Mpaka sasa mabingwa hao wa Ngao ya Jamii wamejikusanyia jumla ya pointi 16 na kujiweka nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi, ikiwa imezidiwa pointi 13 na kinara Simba ambaye yupo kileleni kwa pointi 29.