KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Zeben Hernandez, amesema kuwa ushindi muhimu walioupata jana dhidi ya JKT Ruvu, umefanikiwa kuiweka sawa timu hiyo kwa ujumla baada ya kukosa ushindi kwenye mechi sita zilizopita.

Bao pekee la Azam FC limefungwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ dakika ya 57, kwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa JKT Ruvu, Omary Kindamba, kuunawa mpira ndani ya eneo la 18 kwenye harakati za kuokoa krosi iliyopigwa na Bocco pembeni ya uwanja.

Hernandez ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo kuwa mara baada ya kikosi chake kuvuna ushindi huo, hivi sasa wanachojipanga ni kuhakikisha wanazoa pointi zote 12 katika mechi zao nne zijazo za kumaliza mzunguko wa kwanza watakazocheza kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa.

“Tunamshukuru Mungu kwanza baada ya kupata pointi tatu, kiufupi timu ilikuwa imekosa ushindi kwa kipindi kirefu, ushindi huu kwa kiasi fulani umeiweka sawa timu kuanzia uongozi, wachezaji , mashabiki, tunawapongeza wachezaji kwa kazi kubwa ambayo wamefanya hadi kupata pointi tatu.

“Lakini hilo halitaishia hapo tunaendelea kujipanga na mechi zinazokuja za kutoka nje, kwa hiyo tutawaambia wachezaji na kuwapa mafundisho ili kuweza kupata pointi nyingi zaidi katika mechi hizo zilizobakia,” alisema.

Mabadiliko ya kikosi vs JKT Ruvu

Hernandez pia alizungumzia mabadiliko aliyofanya jana kwenye kikosi cha kwanza kwa kuwaanzisha wachezaji watatu wapya ambao hawakuanza katika mechi zilizopita, ambapo amedai kuwa mabadiliko hayo yaliwasaidia na kufanikiwa kuutawala mchezo.

Mabadiliko aliyofanya ni ya kuwaingiza kikosini beki kinda wa kushoto, Gadiel Michael, aliyechukua nafasi ya Himid Mao aliyecheza nafasi hiyo kwenye mechi mbili zilizopita na sasa alirejeshwa katika eneo lake la kiungo mkabaji, winga Ramadhan Singano, aliyechukua mikoba ya Gonazo Ya Thomas na mshambuliaji Fransisco Zekumbawira aliyecheza mbele sambamba na Bocco.

Michael na Singano walifanikiwa kuleta presha kubwa kwenye lango la Maafande hao kutokana na kasi yao mchezoni na kupiga krosi zao nyingi zenye madhara.

“Mchezo ulikuwa mzuri sana, kubadilisha timu ni kazi ya kocha kwa sababu mbinu ya kwanza inapofeli basi inakupasa uje na mbinu nyingine ili kuweza kupata ushindi na leo tunashukuru tumeweza kupata pointi tatu, wachezaji wote waliokuwa kwenye kikosi changu ni muhimu kwa sababu wamejituma, ukiangalia Gadiel (Michael) amesheza na kajitolea na kiwango chake kimeonekana kuwa kizuri, pia na Messi (Singano) hivyo hivyo naye alicheza na alimiliki vema mchezo.

“Lakini kiufupi bado tatizo ambalo lipo ni lile lile ambapo tunapata nafasi nyingi lakini tunashindwa kuzitumia, lakini ambacho kipo tunaendelea kufanya kazi kwani ni moja ya kazi yetu, tunajaribu kutafuta dawa ya tatizo ili kuweza kuzitumia nafasi kwa wingi kama tunavyozipata ili kuweza kupata mabao mengi,” alisema.

Mechi za Kanda ya Ziwa

Kikosi cha Azam FC kinatarajia kuanza safari ya kuelekea mkoani Kagera kesho Jumatatu Alfajiri kwa ajili ya kujipanga na mechi nne za Kanda ya Ziwa, ikianza kukipiga na Kagera Sugar kwenye mchezo ujao utakaofanyika Uwanja wa Kaitaba mkoani humo, Ijumaa Ijayo Oktoba 28 mwaka huu.

“Kikubwa ambacho kipo ni kuweza kuingia Jumatatu, siku tunayotarajia kusafiri, naamini kikosi ambacho tutakuwa tunacho ni kile ambacho tunakifanyia kazi, tutakipa mafunzo ili kuweza kupata pointi zote ambazo zipo huko ugenini, kikubwa tutahakikisha tunarudi na pointi zote hizo kulinganisha na kazi yetu ambayo tunaifanya,” alisema.

Baada ya kumaliza kazi ya kuiua Kagera Sugar, Mabingwa hao wanaodhaminiwa na kinywaji safi  kinachoburudisha koo na kuchangamsha mwili cha Azam Cola na Benki bora kabisa nchini ya NMB, wataelekea mkoani Mwanza kucheza dhidi ya Toto African (Novemba 2), Mbao FC (Novemba 6), zote zikipigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Azam FC inayoshika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 16 pungufu ya pointi 10 na kinara Simba waliokusanya 26, itakamilisha ratiba ya mzunguko huo, kwa kukipiga na Mwadui katika mechi ya kiporo itakayopigwa Uwanja wa Mwadui, Shinyanga Novemba 9 mwaka huu.

Kauli yake kwa mashabiki

Hernandez alimalizia kwa kuwashukuru mashabiki wa Azam FC kwa sapoti kubwa ambayo wanaendelea kuitoa kwa timu hiyo, licha ya kutokuwa na matokeo mazuri kwa siku za hivi karibuni .

“Tunashukuru sana kwa mchango wao katika kipindi chote ambacho tumepita kwenye wakati mgumu, kwani walikuwa wapo na kutupa sapoti na tunawapa hongera kwa kufanya hivyo, lakini hatuoni kama wamekosea kufanya hivyo kiufupi ni kwamba kwa mashabiki tunawaomba waendelee kuwa wavumilivu kama ambavyo tumeweza kupata pointi tatu leo (jana) tutajitahidi kupata pointi nyingine nyingi kadiri inavyowezekana kwenye michezo inayokuja.

“Bila wao sisi tutajisikia kuwa ni wapweke, tunaamini ya kuwa tutawafurahisha mashabiki na tutaendelea kuwa nao na wao wanapaswa kuendelea kuwa na sisi, wasichoke kwa kwa hali yote ambayo tunapita nayo, cha msingi kuhusu mashabiki waendelee kusapoti timu yao na sisi tutawasapoti kwa kupata matokeo mazuri uwanjani,” alisema.