KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo Jumamosi inatarajia kucheza mechi yake ya mwisho ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex kwa kukipiga na maafande wa JKT Ruvu saa 1.00 usiku.

Mara baada ya mchezo huo, Azam FC itahitimisha mzunguko huo kwa kucheza mechi nne za ugenini Kanda ya Ziwa dhidi ya Kagera Sugar, Toto African, Mbao FC na Mwadui FC kabla ya ligi kusimama kidogo kupisha mashindano mengine na usajili wa dirisha dogo.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na nia moja tu ya kuibuka na ushindi, ikizingatiwa bado haijafanikiwa kupata matokeo mazuri katika mechi sita zilizopita, hivyo licha ya ugumu wa maafande hao wachezaji wa timu hiyo na benchi la ufundi wamejipanga kuondoka na pointi zote tatu.

Uongozi wa timu hiyo kwa ujumla unatambua ya kuwa bado haijafanikiwa kuwafurahisha mashabiki wake kutokana na mwenendo wa kikosi hicho, lakini umekuwa ukifanya kazi kubwa kutatua changamoto zinazojitokeza katika kipindi hiki cha mpito, ambapo unawaomba mashabiki waendelee kuwa pamoja na timu yao kwani wao ni sehemu muhimu sana ya muunganiko wa timu.

Kikosi hicho kimekuwa kikicheza vizuri sana uwanjani na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao, lakini kimekuwa hakina bahati ya kuondoka na matokeo ya ushindi, hii inatokana na nafasi zinazopatikana za mabao kushindwa kutumiwa vema, changamoto ambayo imeendelea kufanyiwa kazi na benchi la ufundi kila siku.

Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi kinachoburudisha mwili na kuchangamsha koo cha Azam Cola na Benki ya bora kabisa nchini ya NMB, itaendelea kumkosa beki wake, Shomari Kapombe, ambaye anasumbuliwa majeraha ya nyama za paja lakini tayari akiwa ameanza mazoezi mepesi tokea juzi.

Pia itamkosa beki wake mwingine David Mwantika, ambaye anaye ametonesha majeraha ya nyama za paja kwenye mazoezi ya wiki hii huku kiungo mkabaji, Jean Mugiraneza ‘Migi’, akikosekana kutokana na kukusanya kadi tatu za njano msimu huu.

Tayari Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, ameshatafuta wachezaji mbadala wa kuziba mapengo yao kwenye mchezo huo.

Rekodi ya mechi zao (H2H)

Huo utakuwa ni mchezo wa 17 timu hizo kukutana kwenye ligi hiyo, ambapo kwa mara ya kwanza zilikutana Septemba 6, 2008 ukiwa ni msimu wa kwanza tokea Azam FC ipande daraja, ilishuhudiwa JKT Ruvu ikishinda mabao 2-1, matokeo ambayo waliyapata pia katika mechi ya mzunguko wa pili msimu huo.

Katika mechi 16 zilizopita, Azam FC imeonekana kuwa na wastani mzuri wa kushinda mechi nyingi pamoja na mabao mengi, imeshinda mara tisa, ikapoteza tatu huku mechi nne zikiisha kwa timu hizo kwenda sare.

Jumla ya mabao 42 yaliyofungwa katika mechi hizo ukiwa ni wastani wa kufungwa mabao 2.6 kwenye kila mechi, Azam FC imefunga robo tatu kati ya hayo ikiweka nyavuni 30 huku JKT Ruvu yenyewe ikitupia 12 tu.

Mchezo wa mwisho kukutana timu hizo kwenye Uwanja wa Azam Complex, ilikuwa ni Mei 4 mwaka huu na ilishuhudiwa ukiisha kwa sare ya mabao 2-2, moja ya mechi ambayo ilitibua malengo ya Azam FC ya kutwaa ubingwa wa ligi msimu uliopita.

Kabla ya kuanza msimu huu, timu hizo zilicheza mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu, ulioisha kwa sare ya bao 1-1, bao la Azam FC likifungwa kwa mkwaju wa pnealti na beki Aggrey Morris huku lile la maafande hao likitupiwa na Atupele Green.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi baada ya kujikusanyia pointi 13, huku JKT Ruvu ikizoa pointi tisa zilizoiweka  kwenye nafasi ya 14.

Rekodi zao zote walipokutana VPL (H2H)

04.05.2016           Azam FC – JKT Ruvu Stars             2 – 2

29.10.2015           JKT Ruvu Stars – Azam FC             2 – 4

07.03.2015           JKT Ruvu Stars – Azam FC             0 – 1

25.10.2014           Azam FC – JKT Ruvu Stars             0 – 1

19.04.2014           JKT Ruvu Stars – Azam FC             0 – 1

13.10.2013           Azam FC – JKT Ruvu Stars             3 – 0

20.02.2013           JKT Ruvu Stars – Azam FC             0 – 4

28.09.2012           Azam FC – JKT Ruvu Stars             3 – 0

01.04.2012           Azam FC – JKT Ruvu Stars             4 – 1

15.10.2011           JKT Ruvu Stars – Azam FC             0 – 2

20.02.2011           JKT Ruvu Stars – Azam FC             0 – 2

29.09.2010           Azam FC – JKT Ruvu Stars             0 – 0

18.02.2010           JKT Ruvu Stars – Azam FC             1 – 1

04.10.2009           Azam FC – JKT Ruvu Stars             1 – 1

24.01.2009           JKT Ruvu Stars – Azam FC             2 – 1

06.09.2008           Azam FC – JKT Ruvu Stars             1 – 2

Total Matches: 16, Goals: 42

*Azam FC: Win- 9, Draw- 4, Lose- 3, Goals- 30

*JKT Ruvu: Win- 3, Draw- 4, Lose- 9, Goals- 12