KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki Kati, Azam FC, imefanikiwa kuutumia vema uwanja wa nyumbani (Azam Complex) baada ya kuichapa JKT Ruvu bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika usiku huu.

Katika mchezo huo, ilishuhudiwa Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, akifanya mabadiliko kadhaa kwa kuwaanzisha wachezaji watatu ambao hawakuanza kwenye mechi zilizopita, ambao ni beki wa kushoto Gadiel Michael, winga Ramadhan Singano ‘Messi’ na mshambuliaji Fransisco Zekumbawira.

Gadiel na Messi walifanikiwa kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo huo wakipeleka presha na langoni mwa wapinzani wao.

Shukrani za pekee zimuendee nahodha wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor’, aliyefunga bao hilo pekee kwa njia ya mkwaju wa penalti dakika 57 baada ya beki wa JKT Ruvu, Omary Kindamba, kuunawa mpira akiwa ndani ya eneo la 18 kwenye harakati za kuokoa krosi iliyopigwa na Bocco pembeni ya uwanja.

Azam FC ilifanikiwa kucheza vema na kutengeneza nafasi nyingine za kufunga mabao, lakini mabeki wa maafande hao walisimama vema kuondoa hatari zote huku baadhi ya nafasi zikishindwa kutumiwa vema na wachezaji wa timu hiyo.

Iliwachukua dakika tano tu za mchezo huo, Azam FC kuweza kufanya shambulizi kali langoni mwa JKT, ambapo pasi safi aliyotoa Bruce Kangwa iliweza kumkuta Bocco ambaye alijaribu kuipatia bao la uongozi timu hiyo baada ya kupiga shuti zuri lililotoka pembeni kidogo ya lango la maafande hao.

Mshambuliaji Fransisco Zekumbawira, aliyeanzishwa sambamba na Bocco katika mchezo huo, naye alipata nafasi nzuri akiwa ndani ya eneo la 18 dakika ya 41 lakini shuti alilopiga lilimlenga kipa wa JKT Ruvu, Said Kipao, ambaye alilidaka vema.

Kuelekea dakika za mwisho mchezo huo, Azam FC ilijikuta ikimaliza mchezo pungufu baada ya kiungo Himid Mao kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi baada ya kumfanyia madhambi mchezaji wa JKT Ruvu.

Kwa ushindi huo muhimu, Azam FC hivi sasa imefikisha jumla ya pointi 16 kwenye msimamo wa ligi ikiwa nafasi ya tano, ambapo mechi nne zinazokuja za kumaliza mzunguko wa kwanza timu hiyo inatarajia kucheza ugenini kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Mabingwa hao wanaodhaminiwa na Benki bora kabisa nchini ya NMB na Kinywaji kinachoburudisha koo na kuchangamsha mwili cha Azam Cola, wataanza kwa kumenyana na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera Oktoba 28 mwaka huu, itakipiga na Toto African (Novemba 2), Mbao FC (Novemba 6), zote zikipigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Kikosi hicho kitakamilisha ratiba ya mzunguko huo, kwa kukipiga na Mwadui katika mechi ya kiporo itakayopigwa Uwanja wa Mwadui, Shinyanga Novemba 9 mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC leo:

Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Daniel Amoah, Aggrey Morris, Himid Mao, Salum Abubakar, Ramadhan Singano/Gonazo Ya Thomas dk 80, John Bocco (C), Fransisco Zekumbawira/Mudathir Yahya dk 51, Bruce Kangwa/Khamis Mcha dk 70