KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Zeben Hernandez, amekiri kwa mara ya kwanza kuwa waamuzi wengi wanaochezesha soka Tanzania wamekuwa wakifanya makosa mengi mchezoni jambo ambalo linaziathiri baadhi ya timu.

Kauli ya Hernandez imekuja saa chache mara baada ya Azam FC kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo.

Mtibwa Sugar ndio ilianza kuwa mbele kwenye mchezo huo baada ya kufunga bao la kushtukiza dakika ya pili likifungwa na Rashid Mandawa kabla ya nahodha wa Azam FC kwenye mchezo wa huo, Himid Mao, kusawazisha kwa mkwaju wa penalti kufuatia Henry Joseph, kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.

“Tunasikitishwa sana na maamuzi ya waamuzi, kwa muda mrefu tokea tumekuja hapa hatujawahi kuzungumzia tatizo hilo, hili ni tatizo kubwa limekuwa likijirudia kila kukicha, inaonekana kwamba kuna kampeni fulani waamuzi wanapewa nafasi wafanye labda kwa sababu ya Azam FC, lakini lazima watambue kuwa hii sio haki.

“Mpira unazungukwa na changamoto nyingi, ukiangalia kwamba waamuzi kuna changamoto nyingi sana ambazo wanazifanya unakuta si tu kwa sababu mchezo unaochezwa uwanjani, bali maamuzi yanaathiri klabu kama klabu, wachezaji wenyewe na hata makocha,” alisema Hernandez.

Kocha huyo alisema kuwa katika maisha yake ya soka yote, hajawahi kushuhudia mchezo ukichezwa kwa dakika chache zaidi kama ule waliocheza jana na Wakatamiwa hao kutoka Manungu, Morogoro.

“Ni kitu cha kushangaza sana kipindi cha pili mpira umechezwa kwa dakika chache sana kuliko muda uliotumika kusimamisha mpira kutokana na wachezaji wa Mtibwa kujidondosha mara kwa mara ili kupoteza muda, lakini mwamuzi alikuwa hawaonyi, sijawahi kuona hata siku moja matukio kama haya katika maisha yangu isipokuwa hapa Tanzania,” alisema.

Ukiachana na upungufu wa waamuzi wa jana wakiongozwa na mwamuzi wa kati, Ahmed Kikumbo kutoka Dodoma, Jumapili iliyopita Azam FC ilinyimwa penalty mbili za wazi kwenye mchezo dhidi ya Yanga baada ya wachezaji wake, John Bocco ‘Adebayor’ na winga Bruce Kangwa kufanyiwa madhambi ya makusudi ndani ya eneo la 18.

Mchezo huo ulichezeshwa na waamuzi Israel Nkongo na wasaidizi wake Frank Komba na Soud Lila, ambaye msimu uliopita alilikataa bao la beki Shomari Kapombe akidai alikuwa ameotea (offside) kwenye sare ya mabao 2-2 dhidi ya Yanga.

Katika hatua nyingine, Hernandez aliendelea kusema bado kuna tatizo kubwa la ufungaji mabao kwenye kikosi chake kwani licha ya kuwachezesha washambuliaji wake wote wane na timu kutengeneza nafasi nyingi, bado wameshindwa kuzitumia vema na hatimaye kupata ushindi.

Kwa mara ya kwanza msimu huu, jana beki wa Azam FC, Pascal Wawa, aliwekwa kwenye orodha ya wachezaji 18 watakaohusika katika mchezo huo, baada ya kupona majeraha na hivyo kuwa miongoni mwa wachezaji wa akiba waliokaa benchi.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki bora kabisa ya NMB na kinywaji safi cha Azam Cola, ilishindwa kuwatumia wachezaji wake wawili tegemeo, beki Daniel Amoah, aliyeumia mkono kwenye mchezo uliopita dhidi ya Yanga baada ya kugongana na kipa wake, Aishi Manula, wakati akiwania mpira pamoja na kiungo Frank Domayo, aliyepata majeraha ya enka katika mazoezi ya mwisho juzi kabla ya kuikabili Mtibwa.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kuteremka kwa nafasi moja hadi ya nane kwenye msimamo ikiwa na pointi 13 sawa na Mbeya City na Ndanda zilizo chini yake, ambapo inatarajia kushuka tena dimbani keshokutwa Jumamosi kuvaana na JKT Ruvu ndani ya Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku.