TIMU ya vijana ya Azam FC chini ya umri wa miaka 20 ( Azam Academy U-20), imedhihirisha kuwa ni moto wa kuotea mbali baada ya jana kuwapa kisago kikali cha mabao 9-1 vijana wenzao wa Jacky’s Academy kutoka Mbagala, Dar es Salaam.

Azam U-20 ilishuka dimbani kwenye mchezo huo wa utangulizi kabla ya Azam FC haijavaana na Mtibwa Sugar jana usiku na kutakata vilivyo na kufanikiwa kuibuka na ushindi huo mnono.

Jacky’s Academy ni kituo cha soka kinachomilikiwa na Meneja wa nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji, Jamal Kisongo.

Vijana hao waliweza kukitumia vema kipindi cha kwanza baada ya kufunga mabao manne ndani ya dakika 27 za mwanzo, yaliyowekwa kimiani na Shaban Idd (dk 5), Sadalah Mohamed (dk 19), Joshua John (dk 25) na Said Mohamed (dk 27).

Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu Idd Cheche, kilizidi kuongeza mashambulizi kipindi cha pili na kufanikiwa kuongeza mabao mengine matano, Idd aliendeleza makali yake kwa kupachika bao la tano dakika ya 50 likiwa ni bao lake la pili kwenye mchezo huo.

Sadalah naye alitupia bao lake la pili dakika mbili baadaye kwa kuipatia timu yake bao la sita, dakika ya 60 alihitimisha hat-trick yake kwa kutupia bao la saba likiwa ni la tatu mchezoni.

Wakati watu wakidhania matokeo yangebakia hivyo, Azam U-20 iliongeza mabao mengine mawili ya haraka dakika ya 77 na 80, yakiwekwa kimiani na John aliyetupia bao lake la pili mchezoni na Rajab Odasi akipigilia msumari wa mwisho.

Hiyo ni sehemu ya michezo ambayo Azam U-20 imekuwa ikiicheza kwa ajili ya kujiandaa na Ligi Kuu ya Vijana ya Taifa, inayotarajia kuanza mwezi ujao ikiwa na udhamini mnono wa Kampuni ya Azam Media Limited inayotoa vingamuzi bora kabisa vya Azam TV.