UNATAKA kuona bonge la surprise waliloandaa wachezaji wa Azam FC ndani ya Uwanja wa Azam Complex? Basi usikose kujitokeza uwanjani kushuhudia mechi ya leo watakapoivaa Mtibwa Sugar saa 1.00 usiku, katika mchezo mkali wa kukata na shoka wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Timu hizo zina historia ndefu ya kuonyeshana upinzani mkali kila zinapokutana, lakini mabingwa wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati wana rekodi nzuri ya ushindi dhidi ya Wakatamiwa hao kutoka Turiani, Manungu, Morogoro.

Kikosi cha Azam FC hivi sasa kina morali kubwa kuelekea mchezo huo, na wachezaji wote kwa ujumla na benchi la ufundi wameonyesha hali ya kujituma mazoezini kwa muda wote wa maandalizi hali inayoashiria wamedhamiria kuondoka na pointi tatu katika mechi hiyo muhimu.

Azam FC imeteleza katika mechi zilizopita, licha ya kucheza kandanda safi na jambo jema zaidi safu ya ulinzi imekuwa ikiimarika kila kukicha dhihirisho la yote ni mechi iliyopita ambapo ilisimama vema na kutoruhusu bao kwenye suluhu dhidi ya Yanga.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, amefanya kazi kubwa wiki hii kunoa makali ya washambuliaji wake baada ya kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza katika mechi zilizopita.

Kuelekea mchezo huo, Hernandez amesema kuwa ni lazima wapate ushindi kuanzia mechi hiyo na ile ya Jumamosi dhidi ya JKT Ruvu, ili kukiongezea morali kikosi hicho kuelekea mechi nne za ugenini.

Mara baada ya mechi hizo mbili za nyumbani, Azam FC itakamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi kwa kucheza mechi nne ugenini, wakianza na Kagera Sugar Oktoba 28 ndani ya Uwanja wa Kaitaba, Kagera.

Mabingwa hao wanaodhaminiwa na Benki bora kabisa nchini ya NMB na Kinywaji kinachoburudisha koo na kuchangamsha mwili cha Azam Cola, watamalizia mechi zao za Kanda ya Ziwa kwa kukipiga na Toto African (Novemba 2), Mbao FC (Novemba 6), zote zikipigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Kikosi hicho kitakamilisha ratiba ya mzunguko huo, kwa kukipiga na Mwadui katika mechi ya kiporo itakayopigwa Uwanja wa Mwadui, Shinyanga Novemba 9 mwaka huu.

Rekodi Azam FC v Mtibwa (H2H)

Hadi hivi sasa timu hizo zimekutana mara 16 kwenye ligi ikiwa na Azam FC ikiwa imeshinda mechi nyingi zaidi ikishinda mara tisa, huku Mtibwa Sugar ikiibuka kidedea mara mbili na ikishuhudiwa mechi tano zikiisha kwa sare.

Azam FC pia imefunga mabao mengi zaidi katika mechi hizo, ambapo katika jumla ya mabao 36 yaliyofungwa, mabingwa hao wa Ngao ya Jamii mwaka huu wameziona nyavu za Mtibwa Sugar mara 25 na Mtibwa Sugar ikifunga mabao 11 tu.

Bao la kwanza la Azam FC ililofunga kwenye mechi ya kwanza ya ligi dhidi ya Mtibwa Sugar ilipopanda daraja mwaka 2008 kwenye ushindi wa bao 1-0, lilifungwa na beki wa zamani wa timu hiyo, Said Sued, Novemba 1, mwaka 2008.

Msimu uliopita Azam FC iliibuka kidedea kwenye mechi zote mbili, ikishinda bao 1-0 nyumbani na ugenini, mabao yote yakifungwa kwa mipira ya adhabu ndogo na nahodha John Bocco ‘Adebayor’.

Bocco, alifunga bao la kwanza dakika za mwisho kwa mpira wa moja kwa moja wa dhabu ndogo ndani ya Uwanja wa Azam Complex huku akitupia jingine kwa mkwaju wa penalti kwenye Uwanja wa Manungu baada ya aliyekuwa beki wa timu hiyo, Andrew Vincent (Yanga), kuunawa mpira wakati akimkabili Kipre Tchetche.

Mechi zote za Ligi walizocheza: 

13th Apr, 2016  Mtibwa Sugar 0-1  Azam FC  

30th Dec, 2015  Azam FC         1-0  Mtibwa Sugar 

11th Apr, 2015  Mtibwa Sugar 1-1  Azam FC

11th Feb, 2015  Azam FC         5-2  Mtibwa Sugar 

25th Jan, 2014  Azam FC         1-0  Mtibwa Sugar

24th Aug, 2013  Mtibwa Sugar 1-1  Azam FC

10th Feb, 2013   Mtibwa Sugar 1-4  Azam FC

22nd Sep, 2012  Azam FC         1-0  Mtibwa Sugar

04th May, 2012 Azam FC         1-2  Mtibwa Sugar

25th Oct, 2011   Mtibwa Sugar 1-0  Azam FC 

13th Mar, 2011 Azam FC         2-2  Mtibwa Sugar 

20th Oct, 2010  Mtibwa Sugar  0-4  Azam FC

25th Feb, 2010  Azam FC         0-0  Mtibwa Sugar

10th Oct, 2009  Mtibwa Sugar  0-1  Azam FC 

15th Mar, 2009 Azam FC         1-1  Mtibwa Sugar

01st Nov, 2008  Mtibwa Sugar  0-1  Azam FC

   

    *Total Matches: 16, Goals: 36

    *Azam FC: Win: 9, Lose: 2, Draw: 5, Goals: 25

    *Mtibwa: Win: 2, Lose: 9, Draw: 5, Goals: 11