KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kesho Jumapili inatarajia kushuka tena dimbani kuivaa Yanga katika mchezo muhimu utakaofanyika Uwanja wa Uhuru kuanzia saa 10.00 jioni.

Azam FC itaingia dimbani ikiwa na nia moja tu ya kusawazisha makosa yaliyotokea kwenye mechi nne zilizopita, kwa kuibuka na ushindi dhidi ya mabingwa hao watetezi wa ligi hiyo.

Mara baada ya kikosi hicho kumalizika mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Stand United, Azam FC imefanya mazoezi makali kwa siku tatu hizi, ambapo benchi la ufundi lilikuwa likifanyia kazi kasoro zilizojitokeza katika mechi zilizopita.

Hadi timu hizo zinaingia dimbani, Azam FC imefanikiwa kujikusanyia jumla ya pointi 11 baada ya kucheza mechi nane ikiwa katika nafasi ya tisa huku Yanga iliyozoa pointi 14 ikiwa nafasi ya tatu.

Kauli ya Kocha Hernandez

Kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa amekiandaa vema kikosi chake kukabiliana na Yanga huku akidai kuwa anaamini watarekebisha makosa waliyofanya kwenye mechi zilizopita na kuibuka na ushindi kesho.

“Matokeo tuliyopata nyuma tumechukulia kama marejeo ya kufanya vizuri katika mchezo wetu wa kesho ambao utakuwa ni mgumu kidogo, lakini kulinganisha na viwango vya wachezaji ambao tunao, naamini tunaweza kurekebisha makosa ambayo yametokeo huko nyuma na kupata pointi tatu katika mchezo huo,” alisema.

Hernandez alisema anaiheshimu Yanga kutokana na historia kubwa waliyokuwa nayo, lakini amedai kuwa kikubwa hataangalia ni mpinzani wa aina gani anacheza naye bali ni anachoangalia ni kushinda mchezo huo.

“Wachezaji watajitahidi kupambana na kucheza vema kwa kutawala mchezo ili kuweza kuhakikisha wanapata ushindi, tumekaa nao na kila mmoja anajua umuhimu wa mchezo huo,” alisema.

Katika hatua nyingine, Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania, aliwaomba mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuvumilia na kuisapoti timu yao huku akiwaahidi mambo mazuri wka kubadilisha mwenendo huo kwenye mchezo wa kesho.

“Mashabiki najua itakuwa ni ngumu kwa upande wao, kutokana na kupoteza mechi zilizopita, tunawaomba wajaribu kuvumilia na kutupa sapoti kwenye timu, tunategemea kwamba kwa mchezo wa kesho tutajaribu kubadilisha matokeo ili Imani yao iweze kuwa kubwa zaidi,” alisema.

Rekodi zao (Head to Head)

Mpaka sasa kwenye mechi za ligi, timu hizo zimekutana mara 16 tokea Azam FC ianze kucheza Ligi Kuu msimu wa 2008/09, ambapo zinafanana kwenye kila kitu kitakwimu.

Katika idadi hizo za mechi, Azam FC imeshinda mechi tano sawa na Yanga huku pia zikienda sare mara sita, jambo la kufurahisha zaidi kila upande umemfunga mwenzake mabao 25.

Hivyo pambano la kesho, linatarajia kuwa la aina yake kama mengine yaliyopita kutokana na upinzani mkali unaotokea kwa timu hizo kila zikimenyana, huku takwimu zikidhihirisha hayo yote.

Msimu uliopita kwenye mchezo wa mwisho timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2, na ile ya mzunguko wa kwanza ikimalizika kwa sara ya 1-1.

Tukiingia kwenye rekodi ya mchezaji mmoja mmoja, nahodha wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, ndiye kinara wa ufungaji mabao kwenye mechi hizo, akitupia mabao 13 kwenye nyavu za Yanga kwenye mechi mbalimbali.

Bocco ametikisa nyavu za Wanajangwani hao mara 10 Ligi Kuu, mara moja Mapinduzi Cup (2012), mara moja tena kwenye mechi ya hisani ya kuchangia walemavu (2011) huku jingine akitupia mwaka huu katika mchezo wa Ngao ya Jamii ulioisha kwa Azam FC kushinda kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya mabao 2-2.