LICHA ya kutengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao, kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kimejikuta kikishindwa kuondoka na ushindi ndani ya Uwanja wa Kambarage, Shinyanga baada ya kufungwa na wenyeji wao Stand United bao 1-0.

Hiyo ni mechi ya nne mfululizo kwa mabingwa hao kushindwa kuibuka na ushindi katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) zinazoendelea, ambapo kwa matokeo hayo inakifanya kikosi hicho kubakiwa na pointi 11 ikiwa nafasi ya nane kwenye msimamo.

Azam FC ingeweza kuibuka na ushindi wa zaidi ya mabao manne leo kama washambuliaji wake wangekuwa makini hasa baada ya kutengeneza nafasi nyingi za wazi za kutikisa nyavu za Stand United.

Timu hizo zote mbili zilijikuta zikishindwa kutambiana kipindi cha kwanza baada ya kutoka uwanjani zikiwa hazijafungana, ambapo kipindi cha pili Azam FC iliingia kwa kufanya mabadiliko ya kumwingiza beki Erasto Nyoni, aliyecheza mechi yake ya kwanza msimu huu kufuatia kupona majeraha huku akitoka mshambulizi kinda, Shaban Idd.

Bao pekee la Stand limefungwa dakika ya 52 na Adam Salamba.

Azam FC ilijitahidi kurejea mchezoni hasa baada ya kuingia mshambuliaji Fransisco Zekumbawira na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambao waliongeza mashambulizi langoni mwa Stand lakini umakini wa kuzitumia vema ulikosekana.

Kikosi cha Azam FC kilichocheza:

Aishi Manula, Ismail Gambo/Salum Abubakar dk 57, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, David Mwantika, Himid Mao, Jean Mugiraneza, Michael Bolou/Fransisco Zekumbawira dk 57, Shaban Idd/Nyoni dk 46, John Bocco (C), Gonazo Bi Ya Thomas