KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kesho Jumatano 10.30 jioni itakuwa kazi moja tu kusaka pointi tatu muhimu pale itakapokuwa ikivaana na wenyeji wao Stand United katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Azam FC iliyobadilika kwa kiwango kikubwa ikicheza soka zuri hivi sasa, inauchukulia kwa uzito mkubwa mchezo huo hasa ikizingatiwa imeteleza katika mechi tatu zilizopita.

Habari njema kuelekea mchezo huo kwa mabingwa hao waliojidhatiti vilivyo msimu huuu, ni kuimarika kwa eneo la ulinzi kufuatia kupona kwa mabeki baadhi ya mabeki wake tegemeo akiwemo Erasto Nyoni.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, ameendelea kufanya kazi kubwa ya kukitengeneza vilivyo kikosi hicho, ambapo wiki hii aliendelea kuziimarisha idara zake mbili sehemu ya ulinzi na ushambuliaji ili kuondoa kasoro ndogo zilizokuwa zikijitokeza katika mechi zilizopita.

Hernandez amesisitiza kuwa japo mchezo utakuwa mgumu lakini amekipanga kikosi chake kupata matokea mazuri ya ushindi hali itakayoongeza morali kwenye kikosi chake kuelekea mechi zijazo.

Hadi Azam FC inaelekea kwenye mchezo huo ikiwa imecheza mechi saba, imefanikiwa kujikusanyia jumla ya pointi 11 katika nafasi sita sawa na Yanga iliyo juu yake na Ndanda iliyokuwa nafasi ya saba baada ya kukipiga michezo nane.

Simba bado imeendelea kukaa kileleni ikiwa na pointi 17, zikifuatiwa na Stand United (16), Mtibwa Sugar (14) na Mbeya City (12), ambazo zimecheza mechi nane kila mmoja.

Rekodi ya kushangaza

Stand United inayoingia kwenye mchezo huo ikiwa haijafungwa mchezo hata mmoja, mpaka sasa inasota kwa mwaka wa pili mfululizo hivi sasa bila kufunga bao lolote dhidi ya Azam FC.

Katika mechi nne za misimu miwili iliyopita tokea Stand United ipande daraja mwaka 2014, Azam FC imeshinda mechi zote kwa asilimia 100 dhidi ya Stand United huku ikifunga jumla ya mabao 8 (ikiwa na wastani wa kupata mabao mawili kwenye kila mechi).

Mara ya mwisho Azam FC kucheza na Stand United ndani ya dimba la Kambarage, ilishinda mabao 2-0 huku Frank Domayo, akifunga bonge la bao la umbali wa takribani mita 35 lililoihakikishia ushindi mabingwa hao, jingine likifungwa na Allan Wanga.