BEKI wa kulia wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Erasto Nyoni, amewaambia mashabiki wa timu hiyo kuwa hivi sasa yupo fiti kurejea uwanjani kukipigania kikosi hicho kwenye mechi mbalimbali zijazo.

Nyoni ameshindwa kuitumikia Azam FC tokea kuanza kwa msimu huu baada ya kuteguka kidole cha mguu wakati wa maandalizi ya msimu Julai mwaka huu, ambapo kwa sasa ameshamaliza programu ya maalumu ya kurejea uwanjani.

Benchi la ufundi chini ya Zeben Hernandez, ambalo limefanya kazi kubwa mpaka sasa kuibadilisha timu kucheza soka la zuri na la kuvutia, jana Ijumaa lilijiridhisha na hali yake baada ya kumjaribu kwenye mechi ya Azam Academy dhidi ya Cosmopolitan iliyoisha kwa ushindi wa mabao 5-1, huku akitoa pande safi lililozaa bao la kwanza.

Nyoni ambaye anamudu kucheza namba zote za ulinzi uwanjani isipokuwa langoni, aliuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa alikuwa anaumia sana kuiona timu yake ikikosa huduma yake baada ya baadhi ya mabeki wengine nao kuwa majeruhi.

“Naendelea kufanya mazoezi kwa nguvu kwa ajili ya kuanza kuisaidia timu yangu ya Azam, hivi sasa narudi nikiwa fiti kabisa kuipigania timu ili kuondokana na hali hii tuliyokuwa nayo kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu.

“Lazima wote tutambue hali tuliyokuwa nayo na kuongeza jitihada binafsi kwa ajili ya timu kusonga mbele na kutokana na hali ninayoiona na mbinu nzuri tunazopewa na makocha wetu ninaimani tutaimarika sana kwa mechi zijazo,” alisema.

Mbali na Nyoni kucheza mechi ya jana kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza, wachezaji wengine wa timu kubwa waliocheza kwa dakika hizo ni kipa Mwadini Ally, beki mwingine aliyemajeruhi Pascal Wawa, viungo Michael Bolou na Masoud Abdallah, winga Ramadhan Singano na washambuliaji Shaban Idd na Fransisco Zekumbawira.

Atoa siri yake ya mafanikio

Beki huyo wa zamani wa AFC ya Arusha na Vital’O ya Burundi, alitaja mambo manne makubwa ambayo yamemfanya kudumu sana kwenye soka akiwa na kiwango chake kile kile pamoja na kuwavutia makocha mbalimbali waliowahi kufanya naye kazi.

“Mambo ambayo yamenifanya kufika hapa nilipo na kudumu kwa muda mrefu kwenye soka ni kujitambua tu kwasababu ni lazima mchezaji yoyote ajitambue, ajiwekee malengo, kujitunza zaidi na kuwa nidhamu kubwa ndani ya nje ya uwanja, hiyo ndio misingi ya mchezaji yoyote kufikia mafanikio na pia kwa anayetaka kucheza muda mrefu kama mimi,” alisema.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji safi cha Azam Cola kinachoburudisha mwili na kulainisha koo, kwa sasa kipo kwenye maandalizi makali kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Stand United utakaofanyika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga Jumatano ijayo (Oktoba 12).