TIMU ya vijana ya Azam FC chini ya umri wa miaka 20 (Azam FC Academy) jioni ya leo imeipa dozi ya mabao 5-1 timu ya Cosmopolitan, mchezo uliofanyika ndani ya viunga vya Azam Complex, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa historia ya soka la Tanzania, Cosmopilitan ndio timu ya kwanza kushiriki michuano ya kimataifa baada ya kuibuka mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 1967 wakati huo ikiwa kwa mfumo wa mtoano, lakini hivi sasa imeporomoka na inshiriki Ligi Daraja la Pili (SDL).

Katika mchezo huo, ilishuhudiwa Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, akiwapima ufiti wa wachezaji wake nane wakiwemo mabeki waliokuwa majeruhi Pascal Wawa na Erasto Nyoni, kiungo Michael Bolou na mshambuliaji Francisco Zekumbawira.

Wengine wakiwa ni kipa Mwadini Ally, kiungo Abdallah Masoud, winga Ramadhan Singano ‘Messi’ na mshambuliaji Shaban Idd, ambao hawajapata muda mwingi wa kucheza msimu huu, wote wakicheza dakika 45 za kipindi cha kwanza ili kurudisha miili yao katika hali ya kawaida.

Wafungaji wa mabao kwenye mchezo huo walikuwa ni Shaban Idd aliyefunga la kwanza na Michael Bolou akipigilia la pili kabla ya mchezo huo kwenda mapumziko.

Kipindi cha pili Azam Academy iliyoonyesha kiwango bora, ilijiongezea mabao mengine kupitia kwa Mohamed Sadalah aliyepiga mawili huku Ramadhan Mohamed akipipiga bao jingine, huku lile la kufuatia machozi la Cosmo likitupiwa na John Alexander kwa njia ya mkwaju wa penalti.

Kabla ya Cosmo kutupia bao hilo, ingeweza kujipatia bao jingine lakini ilishuhudiwa Fakhi Rashid akikosa mkwaju mwingine wa penalty baada ya mpira aliopiga kutoka pembeni ya lango la Azam Academy.

Azam Academy imeendelea kujiweka sawa kupitia michezo mbalimbali ya kirafiki ikijiandaa na Ligi ya Taifa ya Vijana yenye udhamini mnono wa Kampuni ya Azam Media Limited inayotoa vingamuzi bora vya Azam TV.