BEKI chipukizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Gadiel Michael, ameweka wazi kuwa anajifunza mambo mengi sana kupitia Bruce Kangwa wanayecheza naye pamoja nafasi ya beki wa kushoto ndani ya kikosi cha timu hiyo.

Gadiel amekuwa beki mbadala wa mkongwe huyo aliyesajiliwa msimu huu akitokea Highlanders FC ya Zimbabwe, akimudu kucheza namba zote za upande wa kushoto ikiwemo nafasi ya ushambuliaji.

Kangwa hadi anaondoka Zimbabwe baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Zimbabwe, alikuwa kinara wa ufungaji bora kufuatia mabao saba aliyofunga huku akiiacha timu yake ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi.

Akizungumza mapema leo asubuhi na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya timu hiyo, kinda huyo aambaye ni zao la Azam Academy, alisema kuwa baadhi ya mambo anayojifunza kutoka kwa Kangwa ni namna anavyopanda kwa kasi kusaidia mashambulizi na kurejea haraka kukaba.

“Najifunza namna anavyopambana uwanjani muda wote kuisaidia timu na pia anavyopanda kwa kasi kushambulia, unajua mabeki wa pembeni siku zote kushambulia kwa kasi na kurudia kukaba ni mambo muhimu, hivyo hayo yote najifunza sana na inanifanya kuwa na mazoezi yangu binafsi ili kufikia alipo japokuwa hivyo vitu mimi ninavyo, lakini kuna kitu nakiona ni cha ziada sana kwake ambacho kinanifanya nijifunze,” alisema.

Alisema; “Kukaa nje najifunza mengi sana, kwa sababu makocha waliokuja ni wapya pia kuna wachezaji wapya akiwemo mwenzangu tunayeshirikiana naye kwenye namba moja (Bruce Kangwa), kocha amemwamini na kumpa nafasi ninachotakiwa kufanya mimi ni kutokata tamaa ni kujifunza kupitia kwake na kuwa bora zaidi.”

Beki huyo alimalizia kwa kusema kuwa hawezi kukata tamaa bali anachofanya kwa sasa ili kufikia malengo yake na kuwa bora zaidi ni kuendelea kujifunza kupitia kwa Kangwa na kuongeza juhudi na kufikia pale alipo nyota huyo wa timu ya Taifa ya Zimbabwe.