KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Zeben Hernandez, amewaomba mashabiki wa timu hiyo wasichoke kutoa sapoti kwa timu yao kutokana na wao kuteleza katika mechi tatu zilizopita za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Licha ya sare ya mabao 2-2 jana dhidi ya Ruvu Shooting, Azam FC iliweza kuteleza katika mechi nyingine mbili dhidi ya Simba (1-0) na Ndanda (2-1).

Azam FC imekuwa ikicheza soka zuri na kutwala sehemu kubwa ya mchezo hivi sasa chini ya makocha kutoka Hispania wakiongozwa na Zeben, lakini mapungufu machache kikosini yamekuwa yakisababisha kutokea matokeo yasiyotarajiwa na wengi.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Zeben alisema motisha ya mashabiki inahitajika sana kwa ajili ya wao kuibuka na ushindi kama wanavyofanya mashabiki wa timu nyingine mfano Simba na Yanga.

“Jana walikuwa wanatarajia sisi kushinda lakini haikuwa hivyo, hii ni sehemu ya mchezo changamoto zinakuja za hapa na pale, mashabiki wakitupa motisha kwa kuwa pamoja nasi hii itasaidia sana kama timu nyingine zinavyofanya Simba na Yanga na kwa kiasi kikubwa wanamchango mkubwa sana kwenye timu,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania alisema kuwa kadiri ya wao wanavyodhidi kuwasapoti na kutokuvunjika moyo ndio vile ambavyo watakuwa wanasaidia hata wao kuifikisha timu sehemu nzuri huku akiwaahidi kuwa hali itabadilika cha msingi wao ni kuwa na subira.

Maoni vs Ruvu

“Mchezo umemalizika jana, kiufupi tulicheza vizuri na tatizo lililotokea ni namna ya kumaliza mchezo, mara nyingi tumekuwa tukiingia ndani ya eneo la hatari lakini tunashindwa kufunga, kazi kubwa ambayo tunaendelea kuifanya ni kuwapa mafunzo zaidi wachezaji ili kuweza kufikia malengo,” alisema.

Akizungumzia mbio za kufukuzia taji, alisema kuwa: “Malengo yako pale pale kama tulivyopanga, tunaendelea kurekebisha makosa yanayotokea, ukiangalia hata mchezo wa jana si kwamba wale waliotufunga walikuwa na kiwango kikubwa kuliko sisi bali matatizo ya mtu mmoja mmoja ndio yamepelekea wao kutufunga, waliweza kutumia vema nafasi mbili walizopata,” alisema.

Changamoto eneo la ulinzi

Zeben amesema kuwa safu yake ya ulinzi ina changamoto kubwa kutokana na kuumia mara kwa mara kwa wachezaji wa safu hiyo jambo ambalo linawanyima muda wa kufanya mazoezi ya kuzoeana kwa ajili ya kufanya vema kwenye mechi.

“Tatizo la eneo la ulinzi limekuwa kubwa na ambalo halizungumziki kirahisi kwa sababu ukiangalia mabeki wanapaswa kufanya mazoezi pamoja ili kila mmoja aweze kujua udhaifu wa mwenzake na kwenye mechi waweze kusaidiana.

“Lakini ambacho kinatokea hivi sasa kwenye timu yetu ni kwamba mabeki ambao wamecheza jana pengine wanaweza kuwa si wale watakaocheza kesho kwa sababu ya majeruhi, eneo la ulinzi linashindwa kuhamisha wanachokifanya mazoezini na kukileta katika mechi kutokana na tatizo hilo, lakini kikubwa tunaendelea kuwapa maelekezo wale ambao wapo kwa ajili ya kutatua tatizo hilo,” alisema.

Mpaka sasa kwenye eneo hilo, Azam FC imeshindwa kuwatumia ipasavyo mabeki wake Pascal Wawa na Aggrey Morris, ambaye amecheza mechi yake ya kwanza msimu huu dhidi ya Ruvu baada ya kupona majeraha huku Wawa akiwa bado hajawa fiti, walinzi wengine walio majeruhi ni Shomari Kapombe anayesumbuliwa na nyama za paja pamoja na Erasto Nyoni, anayemalizia programu ya mazoezi mepesi kabla ya kuanza kucheza mechi.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji safi kabisa kinacholainisha koo cha Azam Cola, mpaka sasa imejikusanyia pointi 11 katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi, ambapo inatarajia kukipiga dhidi ya Stand United kwenye mchezo ujao wa ligi utakaofanyika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.