UZEMBE uliofanywa dakika za mwisho na safu ya ulinzi ya Azam FC, umeifanya timu hiyo kulazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliomalizika usiku huu.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kucheza mechi tatu mfululizo bila kupata ushindi kufuatia kupoteza michezo miwili ya nyuma yake dhidi ya Simba (1-0) na Ndanda (2-1).

Hiyo inawafanya mabingwa hao kushika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 11 sawa na Yanga iliyo ya nne na Mbeya City katika nafasi ya sita, Simba ipo kileleni kwa pointi 17, wakifuatiwa na Stand United iliyojikusanyia 15 na Mtibwa Sugar wakiwa nazo 13.

Katika mchezo huo ilishuhudiwa beki wa kati wa Azam FC, Aggrey Morris, akicheza kwa mara kwanza msimu huu baada ya kuwa nje ya dimba kwa kipindi cha takribani miezi miwili na nusu akiuguza majeraha.

Azam FC ilibidi itoke nyuma baada ya Ruvu kutangulia kufunga bao la mapema dakika ya nane likifungwa na Fully Maganga akitumia vema makosa ya eneo la ulinzi la timu hiyo kufuatia Jean Mugiraneza kushindwa kupiga kichwa mpira wa juu ambao ulinaswa mfungaji.

Mugiraneza alisawazisha makosa hayo kwa kufunga bao zuri kwa kichwa dakika ya 29 akimalizia kona iliyochongwa vema na Khamis Mcha ‘Vialli’.

Azam FC iliyoonekana kucheza vema kwenye mchezo huo ikitawala sehemu kubwa ya mchezo, ilijikuta ikishindwa kutumia nafasi nyingi ilizotengeneza ambazo zilipotezwa na washambuliaji wake Mcha, nahodha John Bocco na Gonazo Ya Thomas.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika timu zote ziliweza kutoshana nguvu kwa bao moja kila upande, ambapo Azam FC ilianza tena kwa kasi kipindi cha pili ikitaka kupata bao la mapema lakini umakini ulikuwa mdogo kila walipoingia eneo la 18 la timu pinzani.

Alikuwa ni Mcha aliyeweza kuiweka mbele Azam FC akitupia bao la pili dakika ya 70 akiunga kwa shuti mpira uliopigwa kwa kichwa na Shaban Idd aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Bocco, aliyeshindwa kuendelea na pambano kufuatia kupata majeraha.

Kiungo wa zamani wa Azam FC, Shaban Kisiga ‘Maloney’, aliifungia timu yake bao la kusawazisha dakika za mwishoni baada ya kuunasa mpira uliookolewa vibaya na mabeki wa timu hiyo na kufanya mpira huo umalizike kwa sare na timu zote kugawana pointi moja kila mmoja.

Kwa hakika katika mchezo wa leo, beki wa kushoto wa Azam FC, Bruce Kangwa, aliweza kuonyesha kiwango cha hali ya juu akikaba vema, kusaidia mashambulizi kwa kushambulia kwa kasi na kupiga krosi, lakini waamuzi walishindwa kumlinda baada ya kufanyiwa rafu nyingi za makusudi hasa kiungo mwingine wa zamani wa Azam FC, Jabir Aziz, aliyekuwa akikabana naye mara nyingi.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii wanaodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola na Benki ya NMB, wanatarajia kushuka tena dimbani Oktoba 12 mwaka huu kukipiga na Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinnyanga.

Kikosi cha Azam FC:

Aishi Manula, Daniel Amoah, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Jean Mugiraneza, Himid Mao, Khamis Mcha/Ramadhan Singano dk 80, Salum Abubakar, John Bocco (C)/Shaban Idd dk 60, Mudathir Yahya/FrankDomayo dk 72, Gonazo Ya Thomas