“USHINDI ni lazima” Hiyo ndio kauli mbiu ya Azam FC kuelekea mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Ruvu Shooting utakakaopigwa ndani ya Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kesho Jumapili saa 1.00 usiku.

Morali ni kubwa ndani kikosi cha wababe hao wa Afrika Mashariki na Kati, ambapo kila mchezaji ana ari kubwa ya kupigania ushindi katika mchezo huo kufuatia kutopata matokeo mazuri katika mechi mbili zilizopita.

Azam FC inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 10 sawa na Yanga iliyo nafasi ya pili na Mtibwa Sugar nafasi ya tano, iliteleza katika mechi hizo mbili dhidi ya Simba (1-0) na Ndanda (2-1), zote zikifanyika nje ya uwanja wake wa nyumbani (Azam Complex).

Pointi hizo zimepatikana baada ya Azam FC inayozidi kuimarika kila kukicha, kushinda mechi tatu, sare moja na kupoteza mbili huku mpaka sasa ndani ya michezo sita iliyocheza imefunga mabao nane na kuruhusu wavu wake kuguswa matano.

Kati ya mabao nane iliyofunga, nahodha John Bocco ‘Adebayor’, amefunga matatu, wengine ni Mudathir Yahya, Michael Bolou, Khamis Mcha, Gonazo Ya Thomas na Fransisco Zekumbawira waliotupia moja kila mmoja.

Ruvu Shooting kwa upande wao wapo nafasi ya 10 baada ya kutoa sare mbili, ushindi mara mbili na kupokea vipigo viwili, pia wamefunga mabao matano na nyavu zao kutikisika mara saba.

Kocha Mkuu wa mabingwa hao wa Ngao ya Jamii mwaka huu, Zeben Hernandez, amekiweka safi kikosi chake kwa wiki nzima hii akifanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mechi zilizopita na ameweka wazi kuwa ushindi ni muhimu sana ili kuongeza morali zaidi kikosini.

Wachezaji wa Azam FC waliokuwa majeruhi mabeki Pascal Wawa, Aggrey Morris, Erasto Nyoni wameanza kufanya mazoezi na wenzao, wakiwemo pia mabeki wengine Shomari Kapombe, Daniel Amoah na mshambuliaji Fransisco Zekumbawira waliokuwa na majeraha madogo.

Hivyo uamuzi wa nani atacheza na nani atakosekana kutokana na kiasi cha ufiti wao kati ya hao wote, utatolewa na benchi la ufundi kesho kabla ya mchezo huo.

Ikumbukwe kuwa wakati wa maandalizi ya msimu huu, Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na Kinywaji safi cha Azam Cola kinachochangamsha mwili na kusisimua koo, ilicheza mchezo wa  kujipima nguvu na Ruvu Shooting uliofanyika Uwanja wa Mabatini, Pwani na kuisha kwa sare ya bao 1-1, Ibrahima Fofana aliyekuwa kwenye majaribio ndio aliowafungia matajiri hao kwa kichwa huku kiungo mkongwe aliyewahi kukipiga Azam FC, Shaban Kisiga ‘Marlone’ akitupia kwa mpira wa adhabu ndogo ya moja kwa moja. 

Tayari viingilio vya mchezo huo vimeshatangazwa vikiwa ni vya bei chee kabisa, ambavyo ni Sh. 10,000/= kwa jukwaa kuu (VIP) na Sh. 3,000/= kwa mzunguko.

Rekodi zao VPL:

Matches VPL H2H (8):

10-04-2014 Ruvu        0 : 3 Azam FC

02-11-2013 Azam FC 3 : 0 Ruvu

30-03-2013 Ruvu        0 : 1 Azam FC

24-10-2012 Azam FC 1 : 1 Ruvu

18-03-2012 Azam FC 1 : 0 Ruvu

26-09-2011 Ruvu        0 : 0 Azam FC

10-04-2011 Ruvu        1 : 2 Azam FC

06-11-2010 Azam FC 4 : 1 Ruvu

Goals Scored H2H:

Azam FC= 15

Ruvu Sh’ting= 03

Home & Away H2H:

*Azam FC  (H)= Win-3, Draw-1, Lose-0

                  (A)= Win-3, Draw-1, Lose-0

*Ruvu Sh’t  (H)= Win-0, Draw-1, Lose-3

                  (A)= Win-0, Draw-1, Lose-3