KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Zeben Hernandez, ameweka wazi kuwa iwe isiwe ushindi ni muhimu kwa kikosi chake wakati watakapoivaa Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Jumapili ijayo (Oktoba 2, 2016).

Kauli hiyo ya Hernandez imekuja kufuatia Azam FC kuteleza katika mechi mbili zilizopita, ilizofungwa dhidi ya Simba (1-0) kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na Ndanda (2-1) iliyopigwa ndani ya Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara Jumamosi iliyopita.

“Pointi tatu iwe isiwe ni lazima, ni mechi muhimu sana kwetu kwa sababu tumetoka kupoteza mechi mbili na sasa timu inahitaji pointi tatu kwa ajili ya kuweka juu hali ya kujiamini,” alisema Zeben wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz

Alisema jambo zuri kwa kikosi chake ni mmoja wa wapinzani wake, Yanga nayo kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Stand United (1-0).

“Jumamosi hii Simba na Yanga zitakutana, hii ni muhimu kwetu kupata pointi tatu katika mchezo wetu ili kusogelea nafasi ya kwanza, morali ya wachezaji ipo vizuri na matatizo yaliyotokea katika mechi iliyopita ni wachezaji kutopambana ipasavyo, lakini kiwango chetu ni kizuri na kila siku kinapanda,” alisema kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania.

Wachezaji majeruhi

Zeben alisema kuwa kikosi chake kinapitia kipindi kigumu hivi sasa kufuatia takribani wachezaji watano waliokuwa nguzo ya Azam FC msimu uliopita kuwa na majeruhi huku wawili wakiwa wameondoka (Farid Mussa, Kipre Tchetche).

Wachezaji wa Azam FC ambao mpaka sasa ni majeruhi ni mabeki Pascal Wawa, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, huku Daniel Amoah, Shomari Kapombe na mshambuliaji Francisco Zekumbawira, wakiwa na majeraha madogo ambao wanahitaji mapumziko na kufanya mazoezi mepesi kabla ya kuanza kucheza tena.

“Hivi sasa Erasto (Nyoni), Aggrey (Morris) na Wawa (Pascal) tayari wameanza mazoezi na wenzao tokea jana tulipoanza, naamini kwa wiki moja ijayo watakuwa na hali nzuri tayari kwa ushindani, tunafanya kazi ya ziada wiki hii kuhakikisha baadhi yao wanaweza kucheza lakini nitafanya maamuzi ya mwisho Jumamosi ijayo tutakapofanya mazoezi ya mwisho kabla ya kuivaa Ruvu Shooting,” alisema.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji safi cha Azam Cola, imefanikiwa kujikusanyia jumla ya pointi 10 baada ya mechi sita ikiwa katika nafasi ya nne kwenye msimamo sawa na Yanga iliyonafasi ya tatu na Mtibwa Sugar inayokamata tano, Stand United inazo 12 katika nafasi ya pili huku Simba ikiwa kileleni kwa pointi zake 16.