NAHODHA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) wa mwezi Agosti msimu huu.

Bocco anakuwa mchezaji wa kwanza kutwaa tuzo hiyo msimu huu, mpaka sasa akiiongoza Azam FC kushinda mechi tatu, sare moja na kupoteza mara moja katika ligi hiyo iliyofika raundi ya tano.

Straika huyo hatari ametwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wachezaji wengine wawili waliokuwa wakishindanishwa naye ambao ni kiungo wa Simba, Mzamiru Yassin na Said Kipao wa JKT Ruvu.

Katika mechi mbili ilizocheza katika mwezi huo, Bocco aliifungia timu hiyo mabao matatu likiwemo la kusawazisha dhidi ya African Lyon.

Kama hiyo haitoshi, alifunga mabao mengine mawili kwenye ushindi wa mabao 3-0 wa Azam FC dhidi ya Majimaji na timu hiyo kujizolea jumla ya pointi nne kati ya sita katika mechi hizo mbili.

Kwa kuibuka kwake kidedea, Bocco atazawadiwa kitita cha Sh. milioni moja kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo, Kampuni ya Vodacom Tanzania.

Uongozi wa Azam FC unampongeza Bocco kwa mafanikio hayo aliyofikia msimu huu na unapenda kumtakia kila kheri aweze kufanya vema zaidi katika sehemu ya msimu huu uliobakia.