HUKU ikicheza soka zuri na kutawala sehemu kubwa ya mchezo, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, leo imeshindwa kuwa na bahati baada ya kukubali kupoteza mchezo kwa kufungwa na Simba bao 1-0.

Hiki ni kipigo cha kwanza cha timu hiyo baada ya michezo 17 ya ligi kupita, ambapo mara ya mwisho kufungwa ilikuwa Februari 14 mwaka huu ikipoteza dhidi ya Coastal Union bao 1-0 ndani ya Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Pia hii ni mechi ya kwanza kwa Azam FC kupoteza msimu huu ikiwa na makocha kutoka Hispania wanaoongozwa na Kocha Mkuu Zeben Hernandez.

Bao pekee lililoamua matokeo ya mchezo huo, lilifungwa na winga wa Simba, Shiza Kichuya dakika ya 67 akitumia vema uzembe wa kuokoa mpira vibaya uliofanywa kwenye eneo la ulinzi la Azam FC.

Azam FC ingeweza kufunga zaidi ya mabao mawili leo kama safu yake ya ushambuliaji chini ya nahodha John Bocco ‘Adebayor’, Gonazo Bi Thomas, Khamis Mcha, wangeweza kutuliza akili kila mara walipokuwa wakiingia ndani ya eneo la hatari la Simba, ambapo mipira mingi ilionekana kutokaa ndani ya eneo hilo.

Mpaka sasa ukiondoa kupoteza mchezo huo, kikosi cha Azam FC kimeshashinda mechi tatu za ligi na kutoa sare moja dhidi ya African Lyon (1-1), ambapo mchezo ujao inatarajia kukipiga dhidi ya Ndanda FC Jumamosi ijayo (Septemba 24) ndani ya Uwanja wa Nangwanda, Sijaona, Mtwara.

Kikosi kilichocheza leo:

Aishi Manula, Shomary Kapombe, Bruce Kangwa, David Mwantika, Himid Mao, Jean Mugiraneza, Frank Domayo/Mudathir Yahya dk 75, Salum Abubakar, Ya Thomas Renardo/Ramadhan Singano dk 81, John Bocco (C), Khamis Mcha/Francisco Zekumbawira dk 75.