TIMU ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya kituo cha kukuza vipaji cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC ‘Azam FC Academy’ imeendelea vema kujiandaa na Ligi Kuu ya U-20 Taifa baada ya kuichapa Transit Camp mabao 5-1.

Mchezo huo wa kirafiki ulifanyika Uwanja wa Azam Complex jioni ya leo, ambapo ilishuhudiwa kikosi cha Azam Academy kiking’ara vilivyo dhidi ya timu hiyo inashiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL).

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), inaeleza kuwa ligi hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya Azam Media kupitia televisheni yake ya Azam TV inayotesa kwa sasa nchini na kusambaa nchi kadhaa barani Afrika, inatarajiwa kuanza rasmi Novemba mwaka huu ikishirikisha timu za vijana za klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Vijana hao wa Azam walionekana kuanza mchezo huo kwa kasi ya chini hasa kipindi cha kwanza na kujikuta wakienda mapumziko wakiwa na wanaongoza bao moja, lililofungwa dakika ya 40 na Sadalah Mohamed,

Lakini maelekezo waliyopewa na Kocha wao, Idd Cheche, wakati wa mapumziko yalirejesha kasi yao iliyozoeleka na kujikuta wakipata mabao manne kipindi cha pili na kukosa mengine takribani mawili ya wazi.

Nyota wa kikosi hicho anayekuja vizuri, Yahya Zaidi, alikuwa mwiba mchungu kwenye ngome ya ulinzi ya Transit Camp hasa baada ya kufunga ‘hat-trick’ katika kipindi cha pili, akianza kutupia la kwanza dakika ya 51 kwa mkwaju wa adhabu ndogo wa moja kwa moja, likiwa ni la pili kwa Azam Academy.

Yahya alirejea tena nyavuni dakika ya 63 akifunga kwa shuti la kiufundi alipokuwa akimalizia pasi safi ya juu aliyopenyezewa na Uzoka Ugochuku, kiungo fundi wa kikosi hicho Rajabu Odasi alipachika bao la nne dakika ya 66 kwa shuti la chini kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Sadalah.

Transit Camp ilikuja juu na kufanikiwa kupata penalti dakika ya 79 kufuatia kipa Metacha Mnata kumwangusha winga Ahmad Juma kwenye eneo la hatari. Ahmad aliifunga vema penalti hiyo na kuipatia timu yake bao la kufutia machozi.  

Dakika ya 87, Yahya alikamisha hat-trick yake kwa kuifungia Azam Academy bao la tano akimalizia pasi safi kutoka kwa Sadala na hatimaye mpambano huo kumalizika kwa ushindi huo mnono wa vijana hao wa Azam.

Huu ni ushindi wa pili mnono ndani ya wiki moja kwa vijana hao, kwani Jumamosi iliyopita asubuhi waliiadabisha timu nyingine ya FDL, Villa Squad kutoka Kinondoni kwa kuishushia dozi nzito ya 6-0.

Makocha Azam FC waishuhudia   

Makocha wa Azam FC wakiongozwa na Kocha Mkuu, Zeben Hernandez, waliendelea na utaratibu wa kuitupia jicho timu hiyo ya vijana baada ya kuishuhudia mechi hiyo wakiwa sambamba na viongozi wa timu, Makamu Mwenyekiti Nassor Idrissa na Meneja, Phillip Alando.

Zeben na jopo lake wameendelea kuitazama timu hiyo ili kuona vipaji vya timu hiyo, ambapo mara kwa mara amekuwa akisisitiza kuwa moja ya mipango yao ni kuvuna vipaji vinavyofanya vizuri kutoka katika timu hiyo na kuwapandisha kwenye timu kubwa kwa siku za usoni.

Mpaka sasa ameshaanza kuwapa mbinu baadhi ya wachezaji kutoka kikosi hicho, viungo Prosper Mushi, Omary Wayne, Rajabu Odasi, ambao mara kwa mara wamekuwa wakifanya mazoezi pamoja na timu kubwa.

Ukiondoa mshambuliaji Shaban Idd aliyepandishwa msimu uliopita, Zeben amewapandisha wachezaji wengine wawili ambao ni kiungo Abdallah Masoud ‘Cabaye’ na beki Ismail Gambo ‘Kussy Jr’, ambaye alicheza kwa kiwango kikubwa wakati Azam FC ikitwaa taji la Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga mwanzoni mwa msimu huu.     

Moja ya malengo mengine makubwa ya Mhispania huyo ni kuifanya Azam FC kuwa klabu ya mfano Tanzania na timu bora Afrika kuanzia uwanjani kwenye kupata matokeo bora na kucheza soka safi hadi nje ya uwanja.