ZIKIWA zimesalia siku tatu kabla ya kupambana na Simba, Nahodha wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, amesema kuwa wanamorali kubwa ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam Jumamosi ijayo (Septemba 17).

Azam FC inakutana Simba wakati timu hizo zote zikiwa kwenye vita kali kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), zote zikiwa na pointi 10 huku zikitofautishwa na herufi tu za majina baada ya kufanana kwa kila kitu kitakwimu hadi sasa.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi, Bocco alisema kuwa mpaka sasa wanaendelea kupata maandalizi mazuri kutoka kwa makocha wao kuelekea mchezo huo.

“Maandalizi ni mazuri na mazoezi tumeanza vizuri kwa wiki hii, wachezaji wanamorali na tumejipanga kwenda kuchukua pointi tatu dhidi ya Simba, kikubwa tutaenda kupambana na melengo yetu makubwa ni kuibuka na ushindi,” alisema.

Alisema kuanza ligi vema mpaka sasa wakiwa wameshinda mechi tatu na kutoa sare moja, hali hiyo itawaongezea morali wachezaji ya kujiamini mchezoni na hatimaye kuibuka na ushindi katika mchezo huo mkubwa.

Rekodi yake na Simba

Bocco ndiye mshambuliaji pekee nchini mpaka sasa aliyeweza kuzitesa timu za Simba na Yanga kwa kufunga mabao, kila anapokutana nazo katika mechi mbalimbali.

Ukiondoa rekodi ya kuifunga Yanga jumla ya mabao 12, Bocco mpaka sasa amefanikiwa kutikisa nyavu za Simba mara 18 katika mechi za mashindano mbalimbali.

Bocco ataingia kwenye mchezo huo ujao akiwa na morali kubwa ya kuendeleza rekodi yake ya kufunga kwani katika mechi ya mzunguko wa kwanza msimu uliopita alitupia mawili kwenye sare ya 2-2, huku ya wekundu hao yakifungwa na Ibrahim Ajibu.

Akizungumzia rekodi yake hiyo kama ina nafasi, Bocco alisema hawezi kuangalia historia bali anachotaka kukifanya ni yeye kupambana na kufunga mabao katika mchezo huo na hatimaye kuibeba timu yake kuzoa pointi zote tatu.

“Kwa sababu mimi ni mshambuliaji, nikifunga naamini timu yangu itapata pointi tatu, kikubwa kinachonipaga hamasa kwenye mechi hizi kubwa ni wachezaji wenzangu wananipa ushirikiano mzuri na mimi mwenyewe kujituma kwa hiyo najikuta nacheza vizuri na kufunga mabao na kuisaidia timu yangu,” alimalizia.

Bocco ambaye ni mchezaji pekee mwenye rekodi ya aina yake ndani ya Azam FC, ataingia kwenye mchezo huo akiwa yupo kileleni mwa msimamo wa wafungaji bora msimu huu akiwa na mabao matatu sambamba na wacheaji wengine watatu.

Wengine wanaomfuatia ni Rafael Daud (Mbeya City), Laudit Mavugo (Simba) na Hood Mayanja (African Lyon).