KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Zeben Hernandez, amepongeza ari ya kupambana iliyonyeshwa na wachezaji wake katika mechi zote mbili za mkoani Mbeya, huku akidai kuwa sasa mafunzo yao yameanza kuzaa matunda ndani ya kikosi hicho.

Hiyo inatokana na kikosi cha Azam FC jana kukamilisha mechi zake mbili za mkoani Mbeya kwa kuzoa pointi zote sita, hasa baada ya ushindi dhidi ya Mbeya City (2-1) na ule wa kihistoria walioifunga Tanzania Prisons bao 1-0.

Pointi hizo sita zimeifanya Azam FC kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ikiwa na pointi 10, ikiiacha Mbeya City katika nafasi ya pili na pointi zake saba sawa na Yanga na Simba, ambazo zina mchezo mmoja mkononi kila mmoja.   

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo wa jana dhidi ya Mbeya City, Zeben alifurahishwa na kitendo cha kikosi chake kubeba pointi zote sita na kudai safari yao yote ya jijini Mbeya haikuwa bure kutokana na mafanikio hayo.

“Nawashukuru wachezaji kwa sababu mafunzo ambayo wamepokea tokea kipindi tunakuja yanaonekana yanazaa matunda kwa sababu kupata pointi sita ugenini hasa Mbeya ilikuwa ni kama historia.

“Lakini kiukweli kwa sasa hivi imekuwa ni kama kazi rahisi kwa sababu vijana wamejituma sana, na tulichowafundisha ndicho walichoenda kukitekeleza,” alisema.

Aliongeza kuwa : “Kazi imekuwa kubwa sana kwa sababu mpira ambao sisi kama makocha tulitegemea uchezwe, sio ule ambao umechezwa ukilinganisha na hali ya uwanja, lakini pia aina ya mazingira ambayo tumeweza kukutana nayo, ambayo yote ni tofauti sana na yale ambayo tumeyazoea Chamazi.”

Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania, pia alichukua fursa hiyo kuwaelezea wachezaji wapya wa kikosi hicho walioanza kuichezea Azam FC jijini hapa, beki Daniel Amoah na mshambuliaji Gonazo Bi Thomas, akisema kuwa ni wachezaji wazuri.

“Ni wachezaji ambao nao wameonyesha uwezo wao, mazoezi waliyokuwa wakiyapata ingawa kwa kipindi kifupi wamejaribu kuyafanyia kazi, ingawaje kwa wao kazi imekuwa ni ngumu kidogo na hii ni kwa sababu bado hawajaweza kuzoeana na wenzao,” alisema.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB itashuka tena dimbani Septemba 17 mwaka huu kuvaana na Simba.