KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, jioni ya leo imeendeleza moto wake kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kuichapa Mbeya City mabao 2-1 ndani ya Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Ushindi huo umeifanya Azam FC kumaliza mechi zake za mkoani Mbeya kwa rekodi na historia ya aina yake baada ya kuondoka na pointi zote sita kwa mara ya kwanza, hii inatoka na ushindi wa kihistoria walioupata dhidi ya Tanzania Prisons (1-0) kwenye mchezo wa kwanza.

Pointi hizo tatu muhimu zimeifanya Azam FC kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 10 ikiiacha Mbeya City iliyobakia nazo saba kama ilivyo kwa Yanga na Simba, ambazo zenyewe zina mechi moja mkononi kila mmoja.

Dakika chache kabla ya kuanza mtanange huo, benchi la ufundi la Azam FC chini ya Zeben Hernandez, lililazimika kufanya mabadiliko kwenye safu ya ulinzi kufuatia beki David Mwantika, kushtua nyama za paja, tatizo alilopata kwenye mazoezi ya mwisho ya timu hiyo jana.

Mashujaa wa Azam FC katika mchezo huo walikuwa ni Khamis Mcha aliyekuwa kwenye kiwango kizuri leo baada ya kufunga bao la kwanza dakika ya 10 akimalizia mpira uliookolewa vibaya na mabeki wa Mbeya City kabla ya kutengeneza bao la pili kufuatia krosi yake aliyomsetia mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Gonazo Thomas, ambaye alifunga bao la ushindi kwa kichwa sekunde chache kabla ya mpira kwenda mapumziko.

Bao pekee la Mbeya City, iliyoonyesha upinzani mkubwa kwa Azam FC katika mchezo wa leo, lilitupiwa wavuni na kiungo Rafael Daudi dakika 13 kwa mkwaju wa penalti kufuatia mwamuzi Ngole Mwangole, kudai Michael Bolou alimfanyia madhambi Joseph Mahundi ndani ya eneo la hatari wakati wakiwania mpira.

Kutokana na tukio hilo, Bolou alishindwa kuendelea na mchezo huo baada ya kuumia na nafasi yake ikachukuliwa na Frank Domayo.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Azam FC ndio iliyotoka kifua mbele kwa mabao hayo mawili huku wapinzani wao wakiwa nalo moja.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa Mbeya City, ambao walifanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Azam FC, lakini uhodari na upambanaji wa wachezaji wa Azam FC uliweza kuwafanya kulinda lango lao vema hadi mchezo huo ulioshuhudiwa na mashabiki wengi kumalizika.

Kutokana na uwanja kutokuwa katika hali nzuri ya kuruhusu mpira kuchezwa chini, timu zote mbili zilikuwa zikitumia mashambulizi ya mipira mirefu na pasi chache zilizokuwa zikimaliziwa na mipira ya juu.

Rekodi za timu hizo hivi sasa zinaonyesha kuwa, Azam FC imeshinda mechi tano kati ya saba walizokutana kwenye ligi na mbili zikiisha kwa sare.

Mara baada ya mchezo huo kumalizika, kikosi cha Azam FC kitaanza rasmi safari ya kurejea Dar es Salaam alfajiri ya kesho Jumapili, ambapo kikishawasili kitafungua ukurasa mwingine wa kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Simba utakaopigwa Septemba 17 mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC:  

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Bruce Kangwa, Daniel Amoah, Himid Mao, Jean Mugiraneza, Michael Bolou/Frank Domayo dk 17, Salum Abubakar/Shaban Idd dk 81, John Bocco, Khamis Mcha, Gonazo Bi Thomas/Gadiel Michael dk 75