TIMU ya vijana chini ya umri wa miaka 20 (U-20) ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, jioni ya leo imeichapa Vingunguti Rangers bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Mchezo huo ni sehemu ya maandalizi ya kikosi cha vijana hao kutoka Azam Academy kinachojiandaa kushiriki Ligi Kuu ya timu za vijana Tanzania Bara, inayodhaminiwa na Kampuni ya Azam Media, inayomiliki ving’amuzi safi vya televisheni vya Azam TV.

Bao pekee la Azam Academy limefungwa kwa mkwaju wa penati na beki kisiki wa timu hiyo, Abbas Kapombe, ambaye ni mdogo wa nyota wa timu kubwa ‘Azam FC’, Shomari Kapombe.

Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Idd Cheche, anayesaidiana na John Matambara pamoja na Kocha wa Makipa, Idd Abubakar na Meneja Luckson Kakolaki, kipo katika maandalizi makali kujiandaa na ligi hiyo.

Moja ya malengo makubwa waliyojiwekea ni kuendeleza rekodi ya kutwaa makombe ya vijana kwa kubeba taji la michuano hiyo, ambayo imekuja kivingine kabisa tofauti na michuano ile ya awali ya Uhai Cup, iliyokuwa ikidhaminiwa na maji safi ya Uhai yanayotengenezwa kupitia Kampuni ya Bakhresa Group.

Moja ya rekodi kubwa ya timu hiyo kwenye michuano hiyo hadi inafanyika kwa mara ya mwisho, ni kulitwaa taji hilo mara nne huku pia ikiandika rekodi nyingine ya kubeba taji la mashindano ya Rollingstone mwaka juzi pamoja na kombe jingine la Azam Youth Cup ililolitwaa mwaka huu wakati likianzishwa kwa mara ya kwanza.