BAADA ya wachezaji saba wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, kujiunga na timu zao za Taifa, Kocha Mkuu Zeben Hernandez, ametumia mazoezi ya leo Jumatano asubuhi kuwasoma wachezaji wa timu kubwa waliobakia pamoja na wale wa timu ya vijana ‘Azam FC Academy’.

Zeben alitekeleza kazi hiyo kupitia mechi ya mazoezi baina ya timu hizo mbili, iliyomalizika kwa Azam FC kuwafunga wadogo zao mabao 3-0 yaliyowekwa kimiani ni kiungo Mudathir Yahya, mshambuliaji Shaban Idd na winga Ramadhan Singano.

Katika mchezo huo, wachezaji waliokuwa majeruhi Pascal Wawa na Aggrey Morris waliweza kucheza kwa vipindi tofauti, Wawa akiingia kipindi cha pili na Morris akianza mwanzo na kutoka dakika ya 60, wote wakionyesha kuwa wanakaribia kurejea dimbani kutokana na namna walivyocheza.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo uliokuwa mkali na wa aina yake, Zeben alisema mechi hiyo ilikuwa na maana kubwa sana kwake, jambo la kwanza alitaka kuwaangalia wachezaji wake ambao hawajapata muda mwingi wa kucheza.

“Unajua toka tumealiza maandalizi ya msimu, kuna wachezaji wangu hawakupata muda mwingi wa kucheza na wengine hawajacheza kabisa katika mechi zinazoendelea, hivyo nilitaka kuwaangalia na kuwapa nafasi ya kucheza ili kuwaweka fiti,” alisema.

Kuhusu academy

Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania, alisema mbali ya kuwaangalia nyota wake pia alitumia mchezo huo kuwasoma wachezaji wa Azam FC Academy.

“Ni jambo zuri sana kuwajua wachezaji wa academy ya timu unayofundisha, kwani kuna wakati inaweza kutokea kuna majeruhi amepatikana kwenye timu kubwa kabla ya kufikiria kununua mchezaji nje, suluhisho la kwanza litakuwa ni kuangalia mtu anayeweza kuziba pengo ndani ya academy.

“Hivyo nimefurahishwa na vipaji vingi nilivyoviona, lakini kuna baadhi ya mambo ambayo yanatakiwa kurekebishwa ili timu hii iweze kuendana kimfumo na timu kubwa, hili litanirahisishia mimi pale nitakapomchukua mchezaji kutoka chini basi awe ameendana na aina ya soka ninalofundisha huku juu, hivyo natarajia kukaa na kocha wa vijana, Cheche (Idd) ili tuweze kujadili baadhi ya mambo ya kuyafanyia kazi,” alisema.

Zeben alisema kuwa endapo atapewa muda wa kukaa hadi miaka mitatu na kusapotiwa, basi Azam FC itakuwa ni timu ya kiwango cha juu sana kuanzia soka la vijana hadi timu kubwa.

Ili kuonyesha amepania kuwapa nafasi wachezaji vijana kutoka kwenye academy hiyo, Zeben tayari ameanza kuwajumuisha kwenye timu kubwa na kuwapa mbinu mbalimbali wachezaji sita, beki Ismail Gambo, viungo Abdallah Masoud, Rajab Odasi, Omary Wayne, Prosper Mushi pamoja na mshambuliaji Shaban Idd.

Wachezaji wa timu kubwa ambao wapo kikosini hivi sasa wakiendelea na programu hiyo ni, makipa Mwadini Ally, Metacha Mnata, mabeki Wawa, Morris, Gadiel Michael, Ismail Gambo, Bruce Kangwa, viungo Mudathir, Frank Domayo, Michael Bolou, Abdallah Masoud, Singano, wasambuliaji Shaban, Khamis Mcha na Francisco Zekumbawira.