JE, ungependa kujiunga na Azam FC Academy na una umri chini ya miaka 17? Jibu ni moja tu kwa wewe kijana kutoka Wilaya ya Temeke na Kigamboni mwenye kipaji cha soka, tunakuomba ufike kesho Jumapili saa 1.00 asubuhi kwenye makao makuu yetu, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Baada ya kufika ukiwa na cheti chako cha kuzaliwa pamoja na mzazi au mlezi wako, utafanyiwa usajili kabla ya zoezi la majaribio halijaanza rasmi, ambalo litamalizika saa 9.30 jioni.

Azam FC ipo kwenye malengo makubwa ya kujenga timu imara ya vijana wa umri huo baada ya kufanya vizuri kupitia kikosi cha chini ya umri wa miaka 20, ambacho kimemtoa winga Farid Mussa, ambaye muda wowote kuanzia sasa atatimkia Club Deportivo Tenerife ya Hispania kucheza soka la kulipwa.

Vijana pekee ambao wataotakiwa kufika kwenye majaraibio hayo ni wale waliozaliwa kuanzia mwaka 2000, 2001 na 2002, kama haupo kwenye kundi hili basi hautahitajika kwa sasa.

Zoezi hili litasimamiwa kwa ueledi mkubwa na makocha wetu wa timu za vijana, wakiongozwa na Mkuu wa Maendeleo ya Soka la Vijana Azam FC, Mwingereza Tom Legg, ambaye atazunguka mikoa 13 ya Tanzania kusaka vipaji hivyo vinavyohitajika.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Legg aliyataja baadhi ya mambo makuu manne watakayozingatia kwenye majaribio ya vijana hao.

“Jambo la kwanza ni namna anavyoupokea mpira, je anaupokea vizuri? Anaweza kutoa pale tu anavyopokea mpira mara moja (first touch)?, jambo la pili ni uharaka kwenye kufanya maamuzi, je anaweza kufikiria kwa haraka? Anaweza kutoa uamuzi haraka? Anaweza kuutuliza mchezo pale inapohitajika? Anaweza kupandisha kasi ya mchezo pale inapohitajika?,” alifafanua Legg, wakati akieleza vitu viwili vya kwanza vinavyohitajika.

Aliendelea kueleza kuwa: “Jambo la tatu ni tabia ya mchezaji, Je, katika majaribio anaonyesha tabia ya kuwa mtu wa kutaka kujifunza? Na Jambo la nne ni kuwa na ufahamu, ni suala muhimu sana kwa vijana wa umri huo mchanga kuweza kuwa na ufahamu wa kimbinu, Je, anaweza kuusoma mchezo na kuelewa afanye nini? Ni moja ya mambo muhimu sana.”

Legg alielezea kuwa ndani ya academy wanazingatia mambo makubwa matatu ya kuwafundisha wachezaji vijana, la kwanza likiwa ni mpira, la pili tabia na la tatu ni elimu.

“Kunakuwa na mazoezi ya mpira kama ilivyo kawaida kwa klabu zilizo profesheno, pia tunawasaidia kuzijenga tabia zao, namna gani ya kushirikiana na wenzao, uaminifu na ukweli na maadili ya kazi, na suala la mwisho ni kuwapa elimu, kwenye suala hili tunaanzia kuwapa elimu ya kawaida ya shule, kusoma kingereza, hivyo elimu ni jambo la msingi,” alisema.

Mara baada ya mradi huo kumalizika kesho Temeke, joto la Azam FC Academy litahamia Ilala wikiendi ijayo na kumalizia Kinondoni, kabla ya kuzungunguka mikoani wakianzia Zanzibar, Tanga, Morogoro, Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Kigoma, Tabora, Mwanza, Mtwara, Mbeya na kumalizia Iringa.

Ewe kijana mwenye kipaji, endelea kufuatilia mitandao yetu rasmi ya kijamii (website, facebook na twitter) uweze kupata taarifa za kila siku kuhusiana na mradi huu na je, eneo lako litatembelewa lini? Jambo la msingi ni wewe kijana kuandaa vifaa vyako vya majaribio, mzazi au mlezi wako na cheti chako cha kuzaliwa kinachoonyesha taarifa zako mbalimbali.