KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, jioni ya leo imefanikiwa kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kuichapa Majimaji ya Songea mabao 3-0 kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Azam FC iliyopata ushindi wa kwanza kwenye ligi hiyo, ilianza kwa sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza dhidi ya African Lyon, ambapo sasa imekaa kileleni ikiwa na pointi nne ilizojikusanyia sawa na Simba, Tanzania Prisons na Ruvu Shooting, ambazo zinazidiwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa (GD).

Mabingwa hao wanarejea kileleni kwa mara ya kwanza tokea Januari 20 mwaka huu ilipokaa kwa mara ya mwisho baada ya kuichapa Mgambo JKT ya Tanga mabao 2-1, yaliyofungwa na beki Shomari Kapombe, ambapo mpaka sasa zimeshapita siku takribani 220.

Timu hiyo bora iliyoanza msimu huu kwa kutwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Yanga, iliuanza vema mchezo huo ikicheza soka la kueleweka ikionyesha imepania kupata mabao mengi.

Iliwachukua dakika ya pili tu ya mchezo kuweza kuandika bao la uongozi, lililowekwa wavuni kiustadi na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, aliyeiwahi pasi safi ya Kapombe ambaye aliwahadaa mabeki wa Majimaji na kutoa pande hilo.

Bao hilo lilizidi kuwapa nguvu Azam FC, ambao walikuwa wakiliandama lango la wapinzani wao wakitaka kufunga mabao zaidi, lakini mabeki wa Majimaji walikuwa imara kuondoa hatari zote wakiongozwa na kipa wao, Agathon Antony.

Hali hiyo ilifanya kipindi cha kwanza kumalizika kwa Azam FC kwenda mbele na bao hilo, ambapo kipindi cha pili ilirejea na kasi ya kutaka kuongeza mabao mengine huku pia Majimaji ikionekana nayo kubadilika ikitaka kusawazisha.

Dakika ya 55, Azam FC ilifanya shambulizi kali langoni mwa Majimaji na shuti lililopigwa na Mudathir Yahya liliokolewa kwenye mstari na beki wa Majimaji na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, alifanya mabadiliko dakika ya 62 kwa kumpumzisha Ramadhan Singano na kuingia  Khamis Mcha ‘Vialli’, ambaye aliongeza kasi ya mashambulizi ya timu hiyo.

Matunda ya mabadiliko hayo, yaliweza kuipatia Azam FC bao la pili dakika ya 65 lililofungwa na Mudathir, ambaye alimalizia kwa shuti mpira uliotemwa vibaya na kipa wa Majimaji, Aghaton, aliyejaribu kuokoa kwenye mstari shuti lililopigwa na Bocco, ambaye alipokea pasi nzuri ya Mcha.

Hilo ni bao la tatu mfululizo kwa Mudathir kuifunga Majimaji baada ya kutupia mabao mawili msimu uliopita ndani ya uwanja huo, wakati Azam FC ikishinda 2-0.

Azam FC ilizidi kujiimarisha zaidi kwenye eneo la kiungo baada ya kuingia Frank Domayo dakika ya 81, ambaye alijitahidi kufanya kazi ya kusambaza mipira pande zote za uwanja na kukaba.

Sekunde chache baadaye almanusura beki wa kulia Shomari Kapombe, aindikie bao la tatu Azam FC baada ya kupiga shuti kali akiwa nje ya eneo la 18 lililogonga mwamba na kurejea uwanjani.

Dakika ya 82, kipa wa Majimaji Aman Simba, aliyeingia dakika ya 79 kuchukua nafasi ya Aghaton, alifanya kazi kubwa kuokoa shuti kali lililopigwa na Domayo akiwa ndani ya eneo la 18 na kuwa kona.

Kona hiyo iliyochongwa vema na nahodha Himid Mao ‘Ninja’, iliweza kuzaa matunda kwa upande wa wenyeji hao baada ya Bocco kuuwahi mpira wa juu na kufunga kwa kichwa na kuiandikia bao la tatu Azam FC, likiwa ni la pili kwake kwenye mchezo huo.

Bao hilo limemfanya Bocco kuwa kileleni kwenye chati ya ufungaji bora msimu huu akiwa na mabao matatu, aliyofunga ndani ya mechi mbili alizocheza kwa dakika zote tisini, moja jingine alifunga kwenye sare ya 1-1 dhidi ya African Lyon.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kesho Jumapili kabla hakijarejea mazoezini Jumatatu ijayo kuanza maandalizi ya mechi zijazo mbili za ugenini dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons zitakazofanyika mara baada ya wachezaji wa timu za Taifa kurejea.  

Kikosi cha Azam FC:

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Bruce Kangwa, David Mwantika, Jean Mugiraneza, Himid Mao, Michael Bolou, Salum Abubakar/Frank Domayo dk 81, Mudathir Yahya/Francisco Zekumbawira dk 69, John Bocco, Ramadhan Singano/Khamis Mcha dk 62