TIMU ya vijana chini ya miaka 20 ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, jioni ya leo imelazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya kikosi cha Green Warriors, katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Bandari, Temeke, Dar es Salaam.

Huo ulikuwa ni mchezo maalumu wa maandalizi ya msimu mpya kwa timu zote, Azam Academy ikijiweka sawa kwa ajili ya Ligi Kuu ya Vijana huku Warriors inayomilikiwa na Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ikijiandaa na Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara (SDL) na Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

Azam Academy ilianza vema mchezo huo na kutawala asilimia kubwa ya kipindi chote cha kwanza, lakini umakini mdogo wa safu ya ushambuliaji iliyokuwa ikiongozwa na Sadalah Mohamed, iliwakosesha mabao mengi zaidi.

Bao la uongozi la vijana hao lilifungwa na kiungo Ferej Salum, aliyetumia vema uzembe wa mabeki wa Warriors na kupiga shuti la kiufundi lililomshinda kipa na hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Azam Academy ilitoka kifua mbele kwa bao hilo.

Warriors walirejea vema kipindi cha pili na kufanikiwa kuziba mianya ya Azam Academy ya kusaka mabao zaidi baada ya kuonekana kucheza soka la kubutua sana, hali ambayo iliwapa wakati mgumu vijana hao wanaonolewa na Idd Cheche.

Timu hiyo ya jeshi ilifanikiwa kupata bao la kufuatia machozi mwanzoni mwa kipindi hicho kupitia mkwaju wa penalti uliofungwa na Deogratius Kasian na hii ni baada ya beki wa Azam Academy, Joshua kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari wakati akiokoa mpira.

Licha ya kikosi cha Azam Academy kujitutumua kuelekea mwishoni mwa mchezo huo ikisaka bao la ushindi, ilikutana na upinzani mkubwa kutoka kwa kipa wa Warriors, ambaye alipangua mchomo mkali uliopigwa na Sadalah dakika za mwisho na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Moja ya malengo makuu ya Kocha Cheche ya kuutoa mchezo huo kwenye Uwanja wa Azam Complex na kuupeleka Bandari, ni kutaka kuwazoesha wachezaji wake kucheza kwenye kiwanja kibovu na hii mahususi kwa ajili ya kujipanga kisayansi kukipiga katika mazingira yoyote kwenye ligi ya vijana, inayodhaminiwa na Kampuni Azam Media inayotoa ving’amuzi bora vya Azam TV.