NAHODHA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, jana usiku alifunga bao muhimu lililoipa pointi timu hiyo kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya African Lyon uliofanyika Uwanja wa Azam Complex na kuisha kwa sare ya bao 1-1.

Sare hiyo inaifanya Azam FC kuanza ligi ikikamata nafasi ya tano ikiwa na pointi moja sawa na Lyon, Mbao na Stand United, ikiwa nyuma ya Simba, Ruvu Shooting na Tanzania Prisons zilizojikusanyia pointi tatu baada ya kuanza na ushindi.

Lyon ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao la uongozi dakika ya 46 lililokuwa la kushtukiza, akifunga Hood Mayanja, kutupia kwa mpira wa moja kwa moja wa kona upande wa kushoto.

Bao hilo liliishtua Azam FC, ambayo iliamka na kufanya mashambulizi mengi langoni mwa wapinzani wao lakini umakini mdogo uliweza kuwanyima mabao na kujikuta wakimaliza dakika 90 za muda wa kawaida wakiwa nyuma kwa bao hilo.

Azam FC ilibidi isubiri hadi dakika ya tatu ya nyongeza kati ya sita zilizoongezwa na mwamuzi wa mchezo huo, Israel Nkongo kutoka Dar es Salaam, kusawazisha bao hilo kupitia kwa Bocco aliyeitumia vema pasi ya kiungo Abubakar Salum ‘Sure Boy’, na kupiga shuti la kiufundi lililompita kipa wa Lyon, Youthe Rostand.

Mwamuzi huyo alilazimika kuongeza muda huo kufuatia wachezaji wa Lyon kupoteza sana muda tokea kipindi cha kwanza na cha pili wakijiangusha uwanjani huku kipa wao akianguka mara kwa mara hali iliyomalazimu mwamuzi kumuonyesha kadi ya njano kuelekea dakika 20 za mwisho za mchezo huo.

Bao hilo lilizidisha ari kwa upande wa Azam FC kusaka bao la ushindi, lakini hadi mpira huo unamalizika timu zote zilitoka uwanjani na sare hiyo na kila upande ukiondoka uwanjani na pointi moja.

Mwamuzi wa mchezo huo, Nkongo, alimuonyesha kadi ya pili ya njano na kumpa nyekundu beki wa Lyon Hamad Tajiri, baada ya kumfuata mwamuzi huyo na kumzonga mpira ulipomalizika, kadi ya kwanza ya njano aliipata kufuatia kupoteza muda kutokana na kuchelewa kupiga mpira mbele.  

Sare inamaanisha kuwa katika michezo mitano waliyokutana timu hizo, rekodi hivi sasa zinasomeka kuwa Azam FC ineshinda mara tatu, Lyon moja na nyingine moja wametoshana nguvu.

Mara baada ya mchezo huo, Azam FC leo Jumapili asubuhi imefanya mazoezi mepesi ya kurejesha mwili kwenye hali ya kawaida kwa wachezaji waliocheza mechi na wengine wakifanya mazoezi ya kawaida.

Kikosi hicho kesho Jumatatu kitapumzika na Jumanne asubuhi kitaanza rasmi maandalizi ya mchezo ujao wa ligi dhidi ya Majimaji, utakaofanyika Jumamosi ijayo (Agosti 27) kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Vikosi vilivyocheza:

Azam FC: Aishi Manula, Ismail Gambo/Mudathir Yahya dk 46, Bruce Kangwa, Himid Mao, David Mwantika, Jean Mugiraneza, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Shomary Kapombe, Frank Domayo/Kipre Balou dk 63, John Bocco na Shaaban Idd/Francisco Zekumbawira dk 64.

African Lyon: Youthe Rostand, Baraka Jaffar, Khalfan Twenye, Hamad Waziri, William Otone, Omar Salum, Hamad Manzi, Mussa Nampaka, Omar Abdallah/Abdul Hilal dk86, Hood Mayanja na Tito Okello.