KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, leo saa 10.30 jioni itakuwa na kibarua kizito pale itakapokuwa ikivaana na Yanga kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii unaoshiria kufunguliwa kwa pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) 2016/17.

Kikosi cha Azam FC kinaingia kwenye mchezo huo kikiwa na morali kubwa kutokana na maandalizi mazuri iliyofanya chini ya makocha wapya kutoka Hispania, wakiongozwa na Kocha Mkuu Zeben Hernandez.

Ukiachilia mbali ujio wa makocha wapya, pia kuna baadhi ya sura kwa upande wa wachezaji, Azam FC ikiwasajili Wazimbabwe Bruce Kangwa, Francisco Zekumbawire, Muivory Coast Gonazo Bi Thomas, Waghana Enock Atta Agyei na beki kisiki Daniel Amoah.

Rekodi/Takwimu

Hii ni mara ya nne timu hizo kukutana kwa mwaka huu, ambapo Januari walikutana kwenye mchezo wa Kombe la Mapinduzi na kuisha kwa sare ya bao 1-1, mtanange huo ulifuatiwa na ule wa mzunguko wa wa pili wa ligi ambao uliisha kwa sare nyingine ya 2-2 kabla ya Yanga kushinda 3-1 katika fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

Katika hatua nyingine, hii ni mara ya nne mfululizo kwa timu hizo kukutana kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, Yanga ikifanikiwa kuibuka na ushindi mara zote.

Walianza kukutana mwaka 2013, Yanga wakishinda bao 1-0, lililofungwa na Salum Telela, ikashinda tena 3-0 (2014) kabla ya mwaka jana kushinda kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 8-7 kufuatia sare ya 0-0 baada ya dakika 90 za muda wa kawaida kumalizika.

Zeben azungumza

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Zeben alisema amekipanga kikosi chake kushinda mchezo huo huku akiwaomba mashabibi wa Azam FC kufika kwa wingi kushuhudia soka safi.

“Hali ya kikosi ipo vizuri kwani wachezaji wanaelewa na kufuata kile ninachowaelekeza, japo kuna wachezaji nitawakosa  naamini kwa asilimia kubwa tutashinda mchezo wetu,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula ya Hispania alisema: “Kwa mashabiki naweza kuaahidi kuwa kutakuwa na mchezo mzuri dhidi ya Yanga, kulingana na maandalizi makubwa nawaahidi ushindi japokuwa Yanga ni timu nzuri na yenye uwezo mkubwa.”

“Mimi naweka imani yangu yote kwa wachezaji wangu kuliko tambo za wapinzani wetu naamini ya kuwa kikosi hiki kitatuletea ushindi,” alisema.

Himid aungana na Zeben

Kwa upande wake Nahodha Msaidizi wa Azam FC, Himid Mao ‘Ninja’, akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, alisema kuwa wamefanya maandalizi ya nguvu kuelekea mchezo huo na kuahidi kuwa watapambana kuhakikisha wanatwaa ubingwa huo.

“Hali iko nzuri kabisa kwenye kambi yetu, hata mazoezi yetu na wachezaji kwa asilimia 100 wako fiti, kwa hiyo zinapokutana timu mbili siku zote lazima utarajie ushindani mkubwa, ni kitu kizuri pia nafikiri ndoto ya mchezaji yoyote mzuri au timu yoyote nzuri ni kucheza na timu nzuri.

“Unapoishinda timu nzuri unakuwa umedhihirisha uzuri wako, kwa hiyo sisi kama Azam FC ni timu nzuri na tunajipanga kucheza na timu nzuri na tuko vizuri kwa ajili ya kushinda mchezo,” alisema

Kiungo huyo hodari wa ukabaji, mwenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani, naye aliungana na Zeben kwa kuwaomba mashabiki wa Azam FC kujitokeza kwa wingi kushuhudia mambo mapya ndani ya timu hiyo.

“Kama unavyojua kuna vitu vingi vipya vya kuona, tuna mwalimu mpya, kuna baadhi ya wachezaji wapya na vitu vingine zaidi vipya, kwa hiyo waje tu kwa wingi, waje waone Azam FC ya sasa hivi ilivyo tofauti na msimu uliopita pia, waje wasapoti timu pia na waje waangalie mpira mzuri,” alimalizia Himid.

Kauli ya uongozi

Naye Makamu Mwenyekiti wa Azam FC, Nassor Idrissa ‘Father’, alisema kuwa kwa upande wao kiutawala wameshamaliza maandalizi ya mchezo huo na kilichobakia ni wachezaji wao kupigana uwanjani kusaka ushindi.

“Katika ushindani jambo la kwanza lazima uweke asilimia kubwa ya kushinda, ni mapambano makubwa sana timu moja ikitaka kuendeleza rekodi ya kuchukua Ngao ya Jamii na nyingine ikitaka kuchukua kwa mara ya kwanza, tunajua mechi itakuwa kubwa na ngumu na vijana wetu na viongozi tunalijua hilo,” alisema.

“Lakini tuko tayari kwa mapambano na nawaomba na mashabiki nao vilevile ile kazi yao huu ni wajibu wao, ile sapoti yao tunawaomba waiongeze zaidi kwa sababu tulishindwa wote, sasa tunakuja tunataka tujipange tena tusonge mbele pamoja wote, hatuwezi kusema mwaka jana tuliangushwa na wachezaji, hatuwezi kusema viongozi waliangusha timu yetu, hatuwezi kusema mwaka jana mashabiki wetu walituangusha, tulikuwa wote.

“Tulishindwa wote, hatukufika malengo wote, tunajipanga kwa timu yetu ili tuitengeneze tuweze kufikia malengo yetu msimu huu wote kwa hiyo nawaomba, nawahamasisha, wazidi kujiboresha kama walikuwa na aina nyingine ya kucheza na kushangalia waongeze na kuboresha ili tupate kile tunachokitarajia msimu huu,” alimalizia Father.

Mara baada ya Azam FC kumaliza mchezo huo, itaendelea na maandalizi ya kujiandaa na mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya African Lyon iliyorejea kwenye ligi hiyo, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi ijayo (Agosti 20, 2016).