KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imefanikiwa kuufungua msimu mpya wa 2016/17 kwa kutwaa ubingwa wa Ngao ya Jamii baada ya kuichapa Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo.

Hilo ni taji la kwanza la Ngao ya Jamii kwa Azam FC baada ya kulikosa kwa miaka mitatu mfululizo ikipoteza dhidi ya Yanga, pia ni ubingwa wa kwanza kwa makocha wapya kutoka Hispania wa Azam FC wanaoongozwa na Kocha Mkuu, Zeben Hernandez.

Kipindi cha kwanza hakikuwa kizuri kwa Azam FC kutokana na kupwaya kwa eneo la ulinzi, hali iliyopelekea Yanga kupata mabao mawili ya haraka yaliyofungwa na Donald Ngoma.

Ngoma alianza kufunga bao la kwanza dakika ya 20 kwa mkwaju wa penalti kufuatia kuangushwa ndani ya eneo la hatari na beki David Mwantika kabla ya kufunga jingine dakika ya 26.

Azam FC ilijitahidi kurejea mchezoni kuelekea mwishoni mwa kipindi cha kwanza, lakini kulikosekana umakini kwenye eneo la ushambuliaji kila walipolikaribia lango la Yanga,

Mabadiliko yaliyofanywa kipindi cha pili na kocha wa Azam FC, Zeben Hernandez, akiwaingiza kiungo Mudathir Yahya na mshambuliaji Francisco Zekumbawire na kutoka Ramadhan Singano ‘Messi’, Shaaban Idd, yaliongeza uhai kwenye eneo la kiungo la mabingwa hao.

Huku pia akiongeza mashambulizi zaidi kwa kumrejesha katikati kiungo Salum Abubakar aliyekuwa akicheza kama namba saba kipindi cha kwanza pamoja huku akimpeleka pembeni beki Shomari Kapombe aliyeanza mchezo huo kama beki wa kati.  

Zekumbawira, aliyesajiliwa kwenye usajili huu wa dirisha kubwa, alishirikiana vema na Bocco kuwasumbua mno mabeki wa Yanga kwa kupeleka mashambulizi mfululizo, wakibadilishana kushambulia pembeni ya uwanja na katikati.

Juhudi za Azam FC za kulishambulia lango la Yanga zilizaa matunda dakika ya 74 baada ya Kapombe kufunga bao la kwanza kwa shuti la kulala kufuatia kusetiwa mpira na kiungo Jean Mugiraneza ‘Migi’.

Bao hilo lilizidi kuongeza ari zaidi kwa upande wa Yanga na hatimaye ikafanikiwa kupata penalti dakika ya 90 kufuatia beki wa Yanga kuunawa mpira uliokuwa umepigwa na Mudathir na penalti hiyo ilifungwa kiufundi na nahodha John Bocco ‘Adebayor’.

Kufuatia dakika 90 kumalizika kwa sare hiyo, mwamuzi wa mchezo huo Ngole Mwangole kutoka Mbeya, ilibidi aaamue mshindi wa mchezo huo apatikane kwa changamoto ya mikwaju ya penalti kama sheria zinavyotaka.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, ilikuwa imara sana kwenye hatua hiyo kufuatia kufanyia kazi eneo la penalti kwenye mazoezi ya mwisho ya jana, ambapo kwenye mchezo ilifanikiwa kupata penalti zote nne ilizopiga, huku Yanga ikipata moja na kukosa mbili.

Shujaa wa Azam FC kwenye hatua hiyo, alikuwa ni Kipa Bora wa msimu uliopita wa mashindano ya Ligi Kuu na Kombe la FA, Aishi Manula, aliyepangua penalti ya beki Ramadhan Kessy huku nyingine ya Yanga ikikoswa na Haruna Niyonzima aliyegongesha mwamba wa juu na mpira kutoka nje.

Penalti ya kiufundi za Azam FC zilifungwa na Bocco, Nahodha Msaidizi Himid Mao, Kapombe na Michael Bolou, aliyetupia ya mwisho na kuipa ushindi Azam FC.

Baada ya mchezo huo, Azam FC kesho inatarajia kuanza tena mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya African Lyon utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Jumamosi ijayo.

Vikosi vilivyocheza:

Azam FC: Aishi Manula, Isamil Gambo, Bruce Kangwa, David Mwantika, Himid Mao, Jean Mugiraneza, Shomary Kapombe, Salum Abubakar/Michael Bolou dk 90, John Bocco, Shaaban Idd/Mudathir Yahya dk 46 na Ramadhani Singano ‘Messi’/Francisco Zekumbawira dk 46.

Yanga: Deogratius Munishi ‘Dida’, Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Mbuyu Twite, Vincent Bossou, Said Juma, Haruna Niyonzima, Juma Mahadhi/Malimi Busungu dk 81, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe/Simon Msuva dk dk 67, Donald Ngoma.