KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, leo imemaliza michezo ya kirafiki ya kujiandaa na msimu ujao kwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya URA ya Uganda, mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex usiku huu.

Hiyo ni sare ya tatu mfululizo kwa Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji safi cha Azam Cola, baada ya awali kutoshana nguvu na JKT Ruvu (1-1) na Ruvu Shooting (1-1).

Azam FC ilianza vema mchezo huo ikicheza soka la kasi na pasi fupi fupi, lakini tatizo kubwa lililoonekana ni ufungaji wa mabao baada ya washambuliaji Shaaban Idd na Gonazo Bi Thomas aliyeko kwenye majaribio kukosa nafasi kadhaa za kuweka mipira wavuni.

Eneo la kiungo la Azam FC lililokuwa likiundwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Himid Mao ‘Ninja’, Frank Domayo ‘Chumvi’, Masoud Abdallah lilionekana kuwazidi maarifa URA kipindi cha kwanza kutokana na kumiliki sana mipira  huku Waganda hao wakionekana kutumia mashambulizi ya kushtukiza.

Kwenye eneo la mabeki wa kati, kipindi cha kwanza Kocha Mkuu Zeben Hernandez aliwatumia Jean Mugiraneza ‘Migi’ na David Mwantika, huku pembeni upande wa kulia akicheza Shomari Kapombe na kushoto, beki mwenye spidi kali Bruce Kangwa.

Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika timu zote zilishindwa kutambiana kufuati sare ya bila kufungana, ambapo Azam FC iliingia kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko ya wachezaji watano.

Waliotoka ni Kapombe, Thomas, Shaaban, Domayo, Masoud huku wakiingia Ismail Gambo, Francisco Zekumbawire aliyeko kwenye majaribio akitokea Harare City ya nchini Zimbabwe, nahodha John Bocco ‘Adebayor’, Michael Bolou na Mudathir Yahya.  

Mabadiliko hayo yalipunguza kasi ya Azam FC na kujikuta ikifungwa bao la kushtukiza dakika ya 46, lililowekwa kimiani na mshambuliaji wa URA, Bokota Labama.

URA ambao ni mabingwa wa Kombe la Mapinduzi mwaka huu lililofanyika Zanzibar wakiifunga Mtibwa Sugar, ilionekana kuamka kipindi cha pili na kukosa nafasi kadhaa za kufunga mabao, lakini Azam FC ilifanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 73 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Bocco kufuatia beki wa Waganda hao kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari wakati akiokoa mpira uliopigwa na Mudathir Yahya.

Bao hilo lilizidi kuiongezea nguvu Azam FC, hasa baada ya kufanywa mabadiliko mengine ya kutoka Bolou na kuingia Khamis Mcha ‘Vialli’ dakika ya 75, ambapo timu hiyo ilifanya mashambulizi mengi makali langoni mwa URA ili kusaka bao la ushindi.

Nahodha Bocco alifanya kazi ya ziada dakika ya 90 baada ya kushambulia kwa kasi pembeni ya uwanja na kupiga kwa ndani pasi, ambayo iliwapita mabeki wawili na kumkuta Ramadhan Singano ‘Messi’, akiwa ndani ya eneo la hatari na kupiga shuti lililopaa juu ya lango na kufanya mpira huo umalizike kwa sare hiyo.

Huo ndio mchezo wa mwisho wa kirafiki wa Azam FC kabla ya haijaanza msimu ujao kwa kucheza mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, ambao ndio utafungua msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) 2016/17.

Vikosi vilivyokuwa:

Azam FC: Aishi Manula, Bruce Kangwa, Shomari Kapombe/Ismail Gambo dk 46, Jean Mugiraneza, David Mwantika, Himid Mao, Masoud Abdallah/Bolou dk 46/Mcha dk 75, Frank Domayo/Mudathir dk 46, Salum Abubakar/Singano dk 63, Shaaban Idd/Bocco dk 46, Gonazo Bi Thomas/ Zekumbawire dk 46

URA FC: Muwanga Mathias, Ntambi Julius, Sekitto Samuel/Munaaba Allan dk 87, Kawooya Fahad, Kulaba Jimmy, Agaba Oscar, Kagimu Shafik/Kagaba Nicholas dk 71, Lwasa Peter/Elkanah Nkugwa dk 55, Feni Ali/Wandyaka Richard dk 82, Bokota Labama, Lule Jimmy