IKIWA imefikisha mwezi mmoja tokea ianze maandalizi ya msimu ujao, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani jioni ya leo Jumamosi.

Huo ni mchezo wa saba wa kirafiki wa Azam FC, ambao ulikuwa ni mahususi kwa ajili ya benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu Zeben Hernandez, kukiangalia kikosi chake kitakavyokuwa kikitumia mbinu zake kwenye viwanja vibovu.

Walikuwa ni Ruvu waliotangulia kupata bao la uongozi lililofungwa kwa mkwaju wa moja kwa moja wa adhabu ndogo na Shaaban Kisiga.

Azam FC inaodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji cha Azam Cola, ingeweza kupata ushindi mkubwa zaidi ya huo kama si washambuliaji wake, Ibrahima Fofana, Shaaban Idd kupoteza nafasi nyingi za wazi.

Kabla mpira huo haujaenda mapumziko, katika dakika ya 44 Azam FC iliweza kusawaziha bao hilo kupitia kwa Ibrahima Fofana, aliyepiga shuti la kiufundi akiwa pembeni kidogo ndani ya eneo la 18.

Vilevile Azam FC ilianza kumfanyia majaribio mshambuliaji mpya kutoka nchini Ivory Coast, Thomas, ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Fofana.

Mara baada ya mchezo huo kikosi cha Azam FC kesho Jumapili kitakuwa mapumzikoni kabla ya kuendelea na mazoezi kama kawaida Jumatatu ijayo asubuhi.