BAADA ya kukosekana uwanjani kwa muda wa siku 122 (sawa na miezi minne), beki kisiki wa kulia wa Azam FC, Shomari Kapombe, leo amecheza mechi yake ya kwanza tokea apone wakati mabingwa hao wakilazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya JKT Ruvu.

Mchezo huo wa kirafiki ulifanyika ndani ya Uwanja wa Azam Complex, ambapo Kapombe aliingia dakika ya 69 kuchukua nafasi ya kiungo Michael Bolou, ilishuhudiwa mashabiki kadhaa wakimpigia makofi wakati akiingia kama ishara ya kuheshimu urejeo wake.

Mara ya mwisho Kapombe kucheza ilikuwa ni mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika waliocheza na Bidvest Wits ya Afrika Kusini na kushinda mabao 4-3 kabla ya kuugua ugonjwa wa Pulmonary Embolism (donge la damu kuziba mishipa ya damu katika mapafu).

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz , Mtaalamu wa Viungo wa Azam FC, Sergio Perez Soto, alisema Kapombe yuko fiti kwa sasa na anachojaribu kukifanyia kazi ni kumpa dakika chache za kucheza ili kutathimini kiujumla maendeleo yake.

“Kapombe ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa sana, ameanza kucheza vizuri leo akipewa dakika 20 za mwisho, natarajia kuendelea kumwangalia na anaweza kupewa dakika 30 katika mchezo ujao Jumamosi (dhidi ya Ruvu Shooting), lengo letu ni kuona anakuwemo kwenye mchezo dhidi ya Yanga (Agosti 17),” alisema.

Wakati Kapombe akirejea, nyota mpya wa Azam FC Enock Atta Agyei, alipata fursa ya kucheza mechi yake ya kwanza tokea ajiunge na timu hiyo akitokea Medeama ya Ghana wiki iliyopita.

Jambo kubwa la kuendelea kujilaumu kwa Azam FC katika mechi za kirafiki zinazoendelea ni kitendo cha wachezaji kukosa mabao mengi ya wazi, jambo ambalo linamladhimu Kocha Mkuu, Zeben Hernandez, kutafuta dawa ya kutokema suala hilo.

Shujaa wa Azam FC aliyeifungia bao pekee leo ni beki Aggrey Morris, aliyepiga kupitia mkwaju wa penalti kufuatia beki Aziz Gila, kuunawa mpira ndani ya eneo la 18.

Kikosi Azam FC

Aishi Manula/Daniel Yeboah dk 46, Aggrey Morris/Ismail Gambo dk 78, Bruce Kangwa, Himid Mao, Jean Mugiraneza, Michael Bolou/Shomari Kapombe dk 46, Masoud Abdallah, Mudathir Yahya/Frank Domayo dk 62, Shaaban Idd/Khamis Mcha dk 82, Fuadi Ndayisenga/Enock Atta Agyei dk 46, Ibrahima Fofana/Ramadhan Singano dk 62