KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, leo asubuhi imeanza tena mazoezi yake baada ya mapumziko ya jana huku ikitarajia kucheza mechi mbili za kirafiki kwa mujibu wa programu ya wiki hii.

Azam FC ilipumzika jana Jumatatu ili kuondoa uchovu wa kambi ya Zanzibar, ambayo ilikuwa ni sehemu ya muendelezo wa maandalizi ya msimu ujao unaotarajia kuanza Agosti 17, mwaka huu kwa kucheza mchezo wa Ngao ya Hisani dhidi ya Yanga.

Mabingwa hao katika programu ya wiki hii wataendelea kucheza mechi za kirafiki, ambapo kesho Jumatano saa 10.00 jioni itacheza na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Mbali na mchezo huo, Jumamosi ijayo itakipiga na Ruvu Shooting nyumbani kwao kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani, mechi ambayo itafunga maandalizi ya Azam FC wiki hii kabla ya kupumzika Jumapili ijayo.

Mpaka sasa Azam FC imeshacheza mechi tano za kirafiki zote ikishinda kwa kuzilaza, Friends Rangers (2-1), Ashanti United (1-0), Mshikamano (1-0), Wilaya ya Mjini (1-0) na Taifa ya Jang’ombe (1-0).  

Kikosi hicho kinakaribia kufikisha mwezi sasa tokea kilipoanza kufundishwa na makocha wapya kutoka Hispania, Kocha Mkuu Zeben Hernandez, Msaidizi wake, Yeray Romero, Kocha Mkuu wa Viungo, Jonas Garcia, Msaidizi wake, Pablo Borges, Kocha wa Makipa, Jose Garcia na Mtaalamu wa Viungo, Sergio Perez Soto.