BALOZI wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Mh. Hemedi Iddi Mgaza, amevutia na uwezekaji uliofanywa na Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, baada ya kufanya ziara ndani ya makao makuu Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam hivi karibuni.

Mh. Mgaza alifanya ziara hiyo akipokewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, ambaye mbali na kufanya naye mazungumzo pia alipata fursa ya kumtembeza ili kujionea mambo yanayopatikana ndani ya Azam Complex.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuhusu moja ya makubaliano waliyofanya, Mheshimiwa huyo aliahidi kuisaidia timu hiyo kwa kuangalia maeneo ambayo inaweza kunufaika nayo katika mashirikiano na vilabu vilivyo katika maeneo yake ya kiutawala.

“Kwanza nimevutiwa na uwekezaji uliopo hapa, hivyo nipo tayari kuiona Azam FC ikifanya programu na klabu za maeneo hayo hasa nchi ya Qatar, nitaangalia namna gani Azam FC inaweza kupata manufaa katika mashirikiano ya vilabu vingine hususani katika programu za vijana na eneo la masoko katika nchi zilizo katika maeneo yangu ya kiutawala,” alisema Mh. Mgaza.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alimshukuru Mh. Mgaza kwa kuchukua muda wake mwingi na kufika Azam Complex na kujionea mazingira halisi ndani ya timu hiyo.

Mara baada ya ziara yake hiyo, Kawemba alimkabidhi jezi ya Azam FC Mh. Mgaza kama ishara ya kuthamini ujio wake Azam Complex.