KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imeendelea kung’ara kwenye mechi za majaribio za kujiandaa msimu ujao, ambapo usiku wa kuamkia leo Alhamisi imeichapa bao 1-0 Kombaini ya Wilaya ya Mjini iliyopo visiwani hapa Zanzibar.

Mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Amaan saa 2.30 usiku ulishuhudia Azam FC ikitakata vilivyo kwa kuonyesha kandanda safi kipindi cha kwanza ikicheza soka la kasi, pasi na ukabaji wa hali ya juu.

Shujaa wa Azam FC alikuwa ni mshambuliaji Fuadi Ndayisenga, aliyekuwepo kwenye majaribio, ambaye alifunga bao hilo pekee dakika ya 42 kwa ustadi mkubwa akipiga shuti baada ya kuvunja mtego wa kuotea.

Azam FC itabidi ijilaumu yenyewe kwani iliweza kukosa mabao mengi ya wazi hasa kipindi cha kwanza kupitia kwa nahodha John Bocco ‘Adebayor’, Shaaban Idd na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Azam FC iliondoka kifua mbele kwa bao hilo na hata mabadiliko yaliyofanyika kipindi cha pili hayakuweza kuongeza idadi yote ya mabao.

Katika mchezo huo, Kocha Mkuu Zeben Hernandez, alipata fursa ya kumtumia mshambuliaji aliyekuja leo Zanzibar, Mzimbabwe Brian Abbas Amidu, huku wengine watatu wakiwa ni beki wa kushoto, Bruce Kangwa, Ndayisenga na Ibrahima Fofana.

Azam FC inatarajia kucheza mchezo mwingine wa kirafiki Jumamosi ijayo dhidi ya timu ya Taifa ya Jang’ombe utakaofanyika Uwanja wa Amaan.

Kikosi Azam FC:

Daniel Yeboah/Aishi Manula dk 46, Ismail Gambo/David Mwantika dk 46, Bruce Kangwa/Gadiel Michael dk 72, Jean Mugiraneza, Aggrey Morris, Michael Bolou/Khamis Mcha dk 72, Salum Abubakar/Abdallah Masoud dk 60, Mudathir Yahya/Frank Domayo dk 60, John Bocco (C)/Brian Abbas Amidu dk 60, Shaaban Idd/Ibrahima Fofana dk 46, Fuadi Ndayisenga/Ramadhan Singano dk 46