WAKATI mechi mbili za kirafiki za Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC wakiwa hapa kambini visiwani Zanzibar zikiwa zimethibitishwa, habari njema zaidi ni kurejea kufanya mazoezi na wenzake beki wa kulia, Shomari Kapombe.

Kapombe ambaye leo Jumanne asubuhi alianza mazoezi ya uwanjani kwa kufanya mazoezi mepesi ya kukimbia na viungo chini ya uangalizi wa Mtaalamu wa Viungo wa Azam FC, Sergio Perez Soto, jioni aliruhusiwa kwa mara ya kwanza kujumuika na wenzake kwa mazoezi ya kiufundi.

Kama kawaida beki huyo alicheza kwenye namba yake ya beki ya kulia na alionekana akiwa na hamu ya mpira huku akicheza kwa kujiamini zaidi, huku muda mwingi akionekana kufurahia mazoezi hayo yaliyoongozwa na Kocha Mkuu, Zeben Hernandez.

Mtaalamu wa Viungo, Soto aliuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kwa ufupi kuwa: “Kapombe leo ameanza mazoezi ya uwanjani na wenzake na tutaangalia maendeleo yake ndani ya wiki mbili hizi akiwa anacheza uwanjani, siwezi nikasema atacheza lini mechi, hilo linahitaji muda mpaka pale tutakapojiridhisha na maendeleo yake.”   

Kabla ya leo kuanza mazoezi hayo akiwa na beki Erasto Nyoni mwenye maumivu madogo ya enka, Kapombe jana alipewa mazoezi mengi ya viungo ufukweni wakati kikosi cha Azam FC kilipofanya mazoezi katika Ufukwe wa Hoteli ya Kitalii ya Mtoni Marine, ilipofikia timu hiyo.

Mechi mbili Zanzibar

Azam FC imekuja visiwani Zanzibar kwa lengo la kutafuta utulivu wakati Zeben akianza kufundisha mbinu zake kwa wachezaji kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao, katika program hiyo timu hiyo inatarajia kucheza mechi mbili za kirafiki kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam Jumapili ijayo.

Uongozi wa Azam FC umelifanyia kazi suala hilo ambapo wameweza kufanikiwa kupata mechi hizo, ya kwanza itakuwa ni kesho Jumatano saa 2.30 usiku wakipambana na timu ya Kombaini ya Wilaya ya Mjini huku Jumamosi asubuhi ikivaana na timu ya Taifa ya Jang’ombe.