UNAWEZA ukashangazwa lakini huu ndio utambulisho mpya wa beki wa kulia wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shomari Kapombe, ambaye ameamua kuja na staili mpya ya kufuga ndevu zake kuelekea msimu ujao.

Kapombe amewashangaza watu wengi kufuatia staili yake hiyo, aliyoanza kuonekana nayo kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, tokea alipoanza mazoezi mepesi ya gym Jumanne iliyopita.

Beki huyo ameanza mazoezi baada ya kupona ugonjwa wa Pulmonary Embolism (donge la damu kuziba mishipa ya damu katika mapafu), uliokuwa ukimsumbua na kumfanya akae nje ya dimba kwa muda wa miezi mitatu sasa.

Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz kuhusu staili yake hiyo mpya, Kapombe amesema staili hiyo ndio itakayomtambulisha msimu ujao na kudai kuwa hawezi kuzinyoa ndevu hizo mpaka pale atakapofunga ndoa na mchumba’ke aliyekuwa naye sasa.

“Mchumba’ngu ndio kaniambia nifanye hivi, ameniambia napendeza sana nikiwa na ndevu hizi, nasikiliza ushauri wake na nitazinyoa tutakapofunga ndoa hivi karibuni,” alisema.

Kapombe, 23, aliyecheza jumla ya dakika 3188 msimu uliopita, amefuata nyayo za wachezaji mahiri duniani kutoka Argentina, Mchezaji Bora wa Dunia, Lionel Messi na staa wa Manchester City, Sergio Aguero waliowahi kufuga ndevu zao lakini wao wakikamia ubingwa wa Copa America mwaka huu.

Wawili hao waliweka kiapo cha kutonyoa ndevu hizo wakati wakiiongoza Argentina kwenye michuano ya Kombe la Copa America wiki chache zilizopita wakiamini kuwa ni uchawi utakaowapa taji la michuano hiyo na kuondoa mkosi wa kukosa mataji, lakini walishindwa kwa kufungwa na Chile kwa mikwaju ya penalti 4-2 kwenye mchezo wa fainali.